Popular services

KUNDI LA HAMASA LA MEJA LAFANYA DUA YA KUWAOMBEA VIONGOZI, NDUGU NA JAMAA PAMOJA NA TAIFA; KATIBU WA CCM AWAPONDEZA.

 

Na: Nishan Khamis,

Chaani Masingini.

Kundi la Hamasa na Itifaki Meja, Wilaya ya Kaskazini “A”, limefanya dua maalum ya kuwaombea viongozi wa nchi, taifa kwa ujumla, pamoja na wazazi, ndugu na jamaa waliotangulia mbele ya haki. Dua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kudumisha amani, upendo na utulivu nchini.

Akizungumza katika dua hiyo iliyofanyika katika Tawi la CCM Chaani Masingini, Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “A”, Hassan Khatib Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwapongeza vijana wa kundi hilo kwa hatua waliyoichukua. Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahimiza umoja, upendo na mshikamano, na kueleza kuwa kitendo hicho ni kizuri na cha kuigwa, kwani umoja na mshikamano ni msingi muhimu katika harakati zote za maendeleo ya dini na jamii kwa ujumla.

Aidha, aliwasisitiza vijana hao kuendelea kuwaombea dua viongozi wote wa nchi ili waendelee kuwa na afya njema, jambo litakalosaidia kuendelea kuliongoza taifa katika maendeleo yenye tija zaidi.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kaskazini “A”, Ramadhan Masoud Machano, alisema Chama Cha Mapinduzi kina misingi ya umoja, upendo na ushirikiano. Aliongeza kuwa, chini ya usimamizi wake, ataendelea kusimamia misingi hiyo kwa vijana katika harakati zao zote kwa kushirikiana na viongozi wa makundi mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya dini, chama, jamii na taifa kwa ujumla.

Vilevile, alitumia fursa hiyo kuhimiza makundi mengine kuiga utamaduni huo, huku akilitaka Kundi la Meja kuhakikisha kuwa tukio hilo halibaki kuwa mwanzo tu, bali liwe ni sehemu ya mwenendo wao wa kudumu katika nyanja zote, ili kuimarisha zaidi upendo, ushirikiano na umoja miongoni mwa vijana na kwa taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, washiriki wa dua hiyo kutoka makundi mbalimbali wamesema ni wajibu wao kama vijana kuonesha umuhimu wa ushirikiano kwa kuwaombea dua viongozi wa nchi, taifa, pamoja na ndugu na jamaa waliotangulia mbele ya haki. Wamesema kufanya hivyo ni jambo la faraja na lenye maana kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, na kusisitiza kuwa huo ni msimamo wao (itikadi) ambao wataendelea kuudumisha kwa maslahi mapana ya maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla.