Nishan Khamis, Mkoani Pemba
Mwakilishi wa Viti Maalum wa wanawake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kusini Pemba, Maryam Said Khamis, amekabidhi msaada wa bidhaa za vyakula kwa wajasiriamali wa jimbo la Mkoani, hatua inayolenga kuwawezesha kiuchumi na kuimarisha shughuli zao za biashara.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Maryam Said Khamis amesema utoaji wa bidhaa hizo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuwainua wajasiriamali kiuchumi, hususan wanawake.
Amesema lengo ni kuwawezesha wanawake kuendesha maisha yao kwa kujitegemea na kukuza kipato kupitia biashara zao.
Aidha, amewahimiza wanawake kutumia fursa wanazopewa kujikwamua kiuchumi, akisisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi kuhakikisha wananchi wanafikiwa na kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo.
Maryam Said
Khamis amewahakikishia wajasiriamali hao kuwa ataendelea kuwa nao bega kwa bega katika harakati zote za kimaendeleo pamoja na changamoto zinazowakabili, ili kuzitafutia ufumbuzi na kuwaweka katika mazingira bora ya utekelezaji wa shughuli zao za kila siku kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao, wajasiriamali hao wamepongeza msaada walioupata wakisema utawawezesha kukuza mitaji yao, kuongeza vipato na kuboresha maisha yao ya kila siku, huku wakimpongeza Mwakilishi wa Viti Maalum mkoa wa Kusini Pemba, Maryam Said Khamis, kwa moyo wake wa kujali wananchi na juhudi zake za dhati katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkoani, Ali Juma Nassor, amesema hatua hiyo ni ishara ya upendo wa viongozi wa CCM kwa wananchi wao pamoja na dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo.
Jumla ya wajasiriamali 100 wa biashara za vyakula wamekabidhiwa bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni kumi na mbili, zikiwemo mchele, unga wa ngano na mafuta ya kupikia, msaada uliotolewa na Mwakilishi wa Viti Maalum mkoa wa Kusini Pemba, Maryam Said Khamis.

