Popular services

CCM JIMBO LA MKWAJUNI WAFUNGA KAMPENI KWA KISHINDO, WATOA WITO KWA WAPINZANI

 

Na, NISHAN KHAMIS – MACHEPU
JUMAMOSI, 25 OKTOBA 2025

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ali Ame, amewataka vijana na wananchi wa Jimbo la Mkwajuni kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, na kuepuka kulubuniwa na watu wasio na nia njema za kimaendeleo.

Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kushirikiana kulinda tunu ya amani kwa maslahi ya taifa, ili kuendeleza maendeleo endelevu nchini.

Amesema hayo leo katika Uwanja wa Mpira wa Machepu, Jimbo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, wakati wa kufunga kampeni za mikutano ya hadhara kwa kishindo katika jimbo hilo.

Ameeleza kuwa maendeleo yote yanayotekelezwa na viongozi nchini yasingewezekana bila kuwepo kwa amani, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuilinda kama rasilimali muhimu ya taifa.

Aidha, amewataka wananchi kutokubali kuuza utu wao kwa kupoteza tunu ya amani, bali kuwa wamoja katika kuilinda. Ameongeza kuwa CCM imejipanga vizuri kwa uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba, na amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuwachagua wagombea wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais hadi madiwani, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

awali, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Kimkakati ya Jimbo la Mkwajuni, Riziki Pembe Juma, alisema Jimbo la Mkwajuni lina historia kubwa katika siasa za Zanzibar kwa kutoa viongozi wengi wakubwa, hivyo wananchi wana kila sababu kuhakikisha wanaweka alama njema kwa kuwachagua viongozi wote wa CCM.

Wagombea wa jimbo hilo walisema Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 imetekelezwa kwa vitendo kwa zaidi ya asilimia 100, ikigusa sekta za barabara, elimu, kilimo, afya, michezo, na uwezeshaji wa wajasiriamali pamoja na wanafunzi wa vyuo.

Wameahidi kuendeleza kasi hiyo kwa kutekeleza ilani ya mwaka 2025–2030 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, huku wakihamasisha wananchi kuendelea kudumisha amani na umoja nchini.

Baadhi ya wanachama walieleza kuridhishwa kwao na maendeleo yaliyotekelezwa katika jimbo hilo, na kuahidi kulipa fadhila kwa kura za “ndiyo” ifikapo Oktoba 29, huku wakiomba akinamama kuendelee kupewa mikopo zaidi ili kujikwamua kiuchumi.