Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Tumbatu leo, tarehe 7 Oktoba 2025, kimezindua rasmi kampeni zake kwa kishindo, ambapo wanachama na watu wengi mbali mbali waliohudhuria katika mkutano huo.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa mpira wa Donge Mchangani, Wadi ya Kipange, Jimbo la Tumbatu, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Ndugu Iddi Ali Ame, amewataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuwachagua viongozi wote wa CCM ili chama hicho kiendelee kushika dola na kuendeleza maendeleo zaidi katika jimbo hilo.
Amesema kuwa kutokana na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya usimamizi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kupitia utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM 2020–2025, ni vyema wanachama wakaendelea kumuunga mkono kwa kuhakikisha chama kinapata ushindi mkubwa.
Amesisitiza kuwa chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata kanuni na taratibu, hivyo viongozi waliopitishwa na kamati wanapaswa kuonesha umoja, ushirikiano na kudumisha amani — ambayo ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo nchini.
Kwa upande wao, wagombea wa CCM jimbo hilo waliojipambanua kwa kuomba kura, wamesema utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa vitendo umeimarisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, michezo, ajira, uchumi na ujenzi wa miundombinu, jambo linalowapa sababu za msingi kumuunga mkono Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi kubwa alizoonesha katika jimbo hilo.
Aidha, wamesema kuwa kwa kuzingatia Ilani mpya ya CCM ya mwaka 2025–2030, ambayo imejikita katika mikakati endelevu ya maendeleo, watahakikisha wanatekeleza kikamilifu ahadi zake ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Halikadhalika, wametumia nafasi hiyo kuhimiza utunzaji wa amani, upendo na ushirikiano, huku wakisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuichagua CCM ili iendelee kushika dola kwa kishindo na kuimarisha maendeleo zaidi.
Nao baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo wamesema wameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika jimbo hilo. Wameiomba serikali kupitia ilani mpya ya CCM kuendelea kuimarisha jitihada za kuwawezesha wanawake na wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi, kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
