Popular services

CHAUMMA MKWAJUNI WAFUNGA KAMPENI ZA MIKUTANO YA HADHARA KWA KISHINDO, MGOMBEA AAHIDI MAKUBWA.

 


Na, Nishan Khamis – Mkwajuni

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) jimbo la Mkwajuni leo wamefunga kampeni za mikutano ya hadhara katika jimbo hilo kwa kishindo. Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Mkwajuni Mwembe Makuti, mgombea ubunge Haji Abeid Haji kupitia tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma amesema kuna changamoto nyingi kwa wananchi wa jimbo hilo, hivyo endapo watampa ridhaa ya kumchagua atahakikisha anazisimamia changamoto hizo na kupeleka mbele maendeleo zaidi, sambamba na kuibua fursa mbalimbali katika nyanja zote za kijamii, kiuchumi na kijana kwa maendeleo ya jamii ya jimbo hilo.

Haji amesema mfumo wa vyama vingi ni haki ya kikatiba, hivyo suala la maendeleo si kuangalia chama kimoja bali lengo la vyama vyote nchini ni kuongoza dola. Amewaomba wananchi wawe na imani naye kwa kusimamia maendeleo katika jimbo hilo.

Aidha, ameahidi endapo atapata ridhaa ya kuwa mbunge atahakikisha fedha za mfuko wa jimbo zinatumika moja kwa moja na wananchi wenye kuamua kufanya shughuli za maendeleo katika jimbo hilo, kusimamia ipasavyo changamoto za wanawake, vijana hasa ajira, na kukuza pamoja na kurejesha hadhi ya michezo katika jimbo hilo.

Amehimiza wananchi ifikapo Oktoba 29 wajitokeze kwa wingi kumpigia kura za ndiyo kwa mabadiliko ya uongozi wa kimaendeleo katika jimbo hilo, kuondoa utawala uliopo na kuonesha uthubutu wa vijana katika siasa na mageuzi ya kimaendeleo katika jimbo hilo.

Awali, akimkaribisha na kumnadi mgombea huyo, mwenyekiti wa CHAUMMA wilaya hiyo Alawiya Suleiman ametoa pongezi kwa wanawake na vijana kwa muitikio wao katika mkutano huo na kuwaomba kumuunga mkono mgombea huyo ifikapo Oktoba, siku ya uchaguzi, kwa kumchagua na kuwa mbunge wa Mkwajuni kwa maendeleo zaidi.

Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria katika mkutano huo wamesema wanampongeza kwa uthubutu na kujitoa kama kijana na kuonesha ukomavu katika siasa, kwani ni zama za vijana kuzitumia fursa za uongozi nchini, jambo ambalo linastahili kuungwa mkono ifikapo Oktoba 29 ili kumpa nguvu na kuleta mabadiliko ya kisiasa na uongozi katika jimbo hilo kwa maendeleo ya jimbo na Taifa kwa ujumla.