Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Amin Salmin Amour, ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Nungwi, leo ameanzisha kampeni ya “Amka Nungwi Kumekucha” ikiwa na lengo la kuhamasisha amani, utulivu, na maendeleo endelevu. Kampeni hiyo ilifanyika katika Maskani ya ACT-Wazalendo Kigunda, ambapo wagombea wa CCM na wanachama wa chama hicho walikusanyika kwa lengo la kuomba kura za chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa Oktoba 29.
Katika mkutano huo, Ndugu Amin Salmin alikishukuru chama cha ACT-WAZALENDO kwa utulivu na umoja waliouonesha. Aliahidi kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini, kabla na baada ya uchaguzi mkuu, huku akiwahamasisha wananchi wote kuunga mkono viongozi wa CCM katika uchaguzi ujao.
Aidha, baadhi ya wanachama wa ACT-WAZALENDO walieleza utayari wao wa kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha amani inadumu na kuzingatia ahadi walizotoa kuelekea uchaguzi mkuu.

