Na,Nishan khamis-Mkokotoni.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, Mheshimiwa Mattar Zahor Masoud, amewahakikishia wadau wa sekta ya utalii kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili zinashughulikiwa kwa lengo la kuhakikisha ulinzi na usalama wa wageni wanaoingia katika mkoa huo unaimarika, sambamba na kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya utalii.
RC Mattar ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa utalii katika mkoa huo. Mkutano huo ulilenga kusikiliza changamoto na kero wanazokabiliana nazo wadau hao, ili kuweka mikakati bora ya kukuza maendeleo ya sekta ya utalii katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Zanzibar kwa ujumla.
Amesema kuwa, kwa kuwa sekta ya utalii ndiyo inayoingiza pato kubwa la taifa kiuchumi, ni wajibu wa serikali kuhakikisha usalama na miundombinu bora vinakuwepo. Ameongeza kuwa atahakikisha changamoto zote zinazowakabili wadau wa sekta hiyo zinatatuliwa kwa misingi ya maendeleo endelevu ya utalii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na jamii kwa ujumla, ili kuimarisha mikakati ya kukuza utalii. Vilevile amewataka wamiliki wa mahoteli kufuata taratibu sahihi za biashara, ikiwemo kutoa mikataba halali kwa wafanyakazi wao, pamoja na kuhakikisha amani na utulivu, hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu. Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29.
Kwa upande wao, wadau wa utalii wameeleza kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazoathiri sekta hiyo ikiwemo wizi, ukabaji, usumbufu kutoka kwa beach boys, mwendo kasi wa madereva, lugha zisizofaa kwa watalii, uuzaji wa dawa za kulevya, na vitendo vya rushwa. Wadau hao wameomba hatua madhubuti zichukuliwe pamoja na kuimarishwa kwa ulinzi na usalama katika maeneo ya kitalii ili kuepusha vitendo vya kihalifu vinavyoweza kuharibu taswira ya utalii nchini.
Naye Afisa Utalii wa Mkoa huo, Ame Nassor, amesema kuwa Kamisheni ya Utalii kupitia Sheria Namba 6 ya mwaka 2009 imeweka utaratibu wa kuwasimamia shughuli za kitalii, lakini bado kumekuwepo na ongezeko la vijana wanaofanya shughuli hizo pamoja na changamoto za kisiasa katika maeneo ya utalii. Ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza changamoto hizo na kuboresha mazingira ya sekta ya utalii katika mkoa huo.
Kikao hicho kiliwakutanisha wakuu wa wilaya,wakurugenzi,vyombo vya ulinzi na usalama watendaji wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo pamoja na wadau wa utalii mko huo.
