Katika muendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Nungwi, leo ikiwa ni mkutano wa tatu katika jimbo hilo, umevunja rekodi ya mikutano miwili iliyopita baada ya zaidi ya watu elfu moja kujitokeza katika mkutano uliofanyika katika kiwanja cha mpira Kidoti.
Wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla wa jimbo la Nungwi wametakiwa wasikubali kushawishiwa kuingia katika uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, pamoja na kujiepusha na wanasiasa wenye ahadi za uongo zenye nia mbaya kwa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Iddi Ali Ame, wakati akizungumza na wanachama na wananchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo katika Shehia ya kidoti wilaya ya Kaskazini A.
Amesema CCM ndicho chama pekee kinachohubiri amani, mshikamano na upendo nchini, hivyo wananchi wana kila sababu ya kutunza tunu hiyo. Pia amewataka vijana kuacha kushawishiwa na watu wenye nia ya kuvuruga amani kuelekea uchaguzi mkuu.
Aidha, amesisitiza kuwa suala la kura ya mapema ni sheria iliyopitishwa na vyombo vya kutunga sheria nchini, hivyo wananchi wanapaswa kufuata utaratibu huo na kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi ili kuendelea na maendeleo endelevu nchini.
Kwa upande wao, wagombea wa CCM jimbo hilo wamesema kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, mambo mengi yamepangwa kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya nchi, endapo wananchi wataendelea kukiamini chama hicho. Wamesema utekelezaji wa ilani ya mwaka 2020–2025 katika sekta za miundombinu, elimu na afya ni ushahidi wa kazi kubwa iliyofanyika.
Nao, wanachama wa CCM jimbo hilo wamepongeza utekelezaji mkubwa wa zaidi ya asilimia 100 ya ilani ya chama katika eneo hilo, huku wakiomba wanawake kuendelea kupatiwa mikopo zaidi na kushirikishwa ipasavyo katika nyanja zote za kimaendeleo nchini.
