Nishan Khamis, Zanzibar.
“Nimeingia katika jimbo hili kwani tangu awali limekuwa likiongozwa na viongozi wa kiume nimekuja kuonesha kuwa wanawake na sisi tunaweza,” amesema kwa tabasamu Asha Said Suleiman, mgombea wa uwakilishi wa Jimbo la Mtambile kupitia chama cha Alliance for Democratic Change (ADA-TADEA).
Ni kauli yenye uzito inayodhihirisha dhamira ya mwanamke huyu ambaye si tu anapigania nafasi ya uongozi, bali pia anasimama kama ishara ya matumaini kwa wanawake na vijana wa Pemba, safari ya Asha si ya kutafuta umaarufu, bali ni ya kujenga jamii yenye usawa na haki,amejikita katika kupigania maendeleo ya wanawake, vijana na watoto, akiamini kuwa jamii imara hujengwa kwa kuwapa nafasi wote bila ubaguzi.
Asha alizaliwa mwaka 1976 katika kijiji cha Msingini, Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba ni mama wa watoto watano na pia ni mfanyabiashara mwenye juhudi ambaye amekuwa mfano wa mwanamke anayejituma katika kila nyanja za maisha.
Safari yake ya kisiasa ilianza rasmi mwaka 2014 alipojiunga na chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo). Mwaka 2015, alijitosa kugombea nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Mkoani, hatua iliyompa uzoefu mkubwa katika ulingo wa siasa. Hata hivyo, safari hiyo haikuwa rahisi kwani alifukuzwa chamani kwa kufuata agizo la serikali kukubali kurejelewa kwa uchaguzi, jambo lililokwenda kinyume na msimamo wa chama hicho wakati huo.
Baada ya hapo, mwaka 2017 alijiunga na Chama cha Wananchi (CUF) na kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini na mwaka 2020 aligombea tena nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Mtambile kupitia chama hicho, lakini mwaka 2024 aliamua kujiondoa kutokana na kutoridhishwa na sera zake.
Mwaka 2025, Asha alichukua hatua mpya kwa kujiunga na Alliance for Democratic Change (ADA-TADEA) baada ya kuvutiwa na sera zake zinazosisitiza usawa wa kijamii, ujumuishi, na maendeleo ya wanawake na watoto. Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mjumbe mkuu wa taifa, na mgombea wa uwakilishi wa jimbo la Mtambile.
Kama mwanamke anayejitosa kwenye ulingo wa siasa, Asha anakiri kwamba safari yake haijakuwa rahisi, anakumbuka changamoto nyingi alizokutana nazo ikiwemo udhalilishaji wakati wa kampeni hasa zile kampeni za nyumba kwa nyumba na ukosefu wa rasilimali fedha ni kikwazo kufikia malengo ya kisiasa.
“Changamoto kubwa niliyokumbana nayo ni udhalilishaji na ukosefu wa rasilimali fedha lakini nimepata sapoti kubwa kutoka kwa wanawake wenzangu na watoto wangu, ambao wananipa nguvu ya kuendelea kupambana,” amesema akiwa na tabasamu la matumaini.
Wakati mwingine, amesema, amekutana na maneno ya kudhalilisha kutoka kwa baadhi ya watu wanaoamini kuwa siasa ni za wanaume pekee. Hata hivyo, anachukulia hali hiyo kama changamoto inayompa nguvu zaidi ya kuthibitisha uwezo wa mwanamke katika uongozi.
Baadhi ya majirani zake wameonesha kumkubali na kumuunga mkono katika harakati zake, wakisema kuwa ni mwanamke mwenye moyo wa kujituma na asiyeogopa kusimamia anachokiamini.
Asha amesema sababu kubwa ya kuingia katika siasa ni kuona wanawake, vijana na watoto wakikabiliwa na changamoto nyingi ndani ya jamii.
“Nimeona wanawake bado wapo nyuma na wengi wanaogopa kukimbilia fursa za uongozi. Nimeamua kuwa mfano kwa wengine ili kukomesha mfumo dume unaoamini kuwa mwanamke hana sifa za kuwa kiongozi,” amesema kwa msisitizo.
Ameeleza kuwa anapogombea, haoni tu nafasi ya madaraka bali fursa ya kuwatetea wale wasio na sauti. Kwa mtazamo wake, siasa ni jukwaa la kuleta mabadiliko chanya, kuhimiza usawa wa kijinsia na kuhakikisha kila mwananchi anapata haki zake za msingi.
Kati ya nguzo kubwa zinazompa nguvu Bi Asha ni familia yake. Watoto wake wamekuwa chanzo cha motisha na uthubutu.
“Watoto wangu wananipa nguvu kubwa ya kuendelea wananitia moyo kila mara ninapokutana na changamoto. Wamekuwa sehemu ya safari yangu ya kisiasa,” amesema kwa upole.
Mtoto wake wa kiume pekee, Annual Khatib ambaye , amesema anajivunia sana kuwa na mama jasiri kama Asha.
“Mama yangu ni mwanamke shupavu na mwenye mapenzi makubwa kwa familia na jamii, mimi nipo bega kwa bega naye kumpa nguvu hadi afikie malengo yake katika siasa na uongozi”.
Kwa upande wake, Yumna Ahmed Khalid, mtoto wa kike wa Asha, amesema mama yao ni kielelezo cha ujasiri na mlezi bora katika familia yao na wanajivunia kwa ushupavu mama yao ns wataendelea kumuunga mkono katika harakati zake zote ili atimize malengo yake.
Mbali na siasa, Asha pia ni mfanyabiashara anayejituma kuhakikisha familia yake inapata mahitaji ya kila siku,amesema siasa njema ni ile inayojengwa juu ya misingi ya amani, umoja na ushirikiano.
“Ni wajibu wa kila mwanasiasa kuhakikisha tunalinda amani, maana hiyo ndiyo tunu kubwa ya taifa letu,” amesema kwa utulivu.
Ameziomba taasisi kama UN Women, Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania(TAMWA–ZNZ), Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA), Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), pamoja na mashirika mengine, kuendelea kuwasaidia wanawake wanaojitokeza kugombea kwa kuwapatia elimu ya uongozi, msaada wa kifedha, na motisha ya kijamii.
“Elimu ya uongozi ni muhimu sana kwa kuwajenga wanawake kuwa viongozi imara, wenye kujiamini na kuthubutu kufikia ndoto zao,” amesisitiza kwa tabasamu.
Leo hii, Asha Said Suleiman anaendelea na kampeni zake za kugombea uwakilishi wa Jimbo la Mtambile, akiwa na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Ni mwanamke ambaye amedhihirisha kuwa uongozi si wa wanaume pekee bali ni wa yeyote mwenye nia, uwezo na moyo wa kuitumikia jamii.
Kwa tabasamu la matumaini, amesema,
“Safari yangu bado inaendelea, na naamini wanawake wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla watafikia ndoto zao pale tutakapoungana na kuamini kuwa tunaweza.”


