Popular services

ZEC YASISITIZA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI KUFANYA KAZI KWA UFANISI

 


Na Nishan Khamis Gamba, Kaskazini Unguja

Kamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Juma Haji Ussi, amewataka wasimamizi wa uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini A kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na mafunzo wanayopatiwa, ili kufanikisha zoezi la uchaguzi kwa ufanisi, uwazi na amani kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Kamishna huyo ametoa  wito huo katika kijiji cha Gamba, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo. Amesema ufanisi wa tume unategemea utekelezaji mzuri wa taratibu zote za uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya kisheria, maelekezo na elimu wanayopata katika mafunzo hayo.

Ameeleza kuwa wasimamizi hao wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, nidhamu na uadilifu, sambamba na kuimarisha mahusiano mazuri na viongozi wa shehia katika maeneo yao, ili kuhakikisha uchaguzi unakamilika kwa salama na amani.

Aidha, Kamishna Ussi amewapongeza wasimamizi hao kwa kuteuliwa katika nafasi hizo muhimu za kitaifa na amewataka kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tume ya Uchaguzi Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Afisa Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini A, Jaala Makame Haji, ametoa shukrani kwa Kamishna huyo kwa maelekezo na nasaha zake, akieleza kuwa wilaya hiyo ina jumla ya shehia 44, vituo vya kupigia kura 185, na vituo vitano vya awali vya kupigia kura.

Amesema maandalizi yote yatafanyika kwa umakini na ufanisi ili kuhakikisha mafanikio ya tume na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Wasimamizi wa uchaguzi waliochaguliwa wameahidi kufanya kazi kwa moyo wa kizalendo, weledi na ushirikiano ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanikiwa kwa salama na amani nchini.