Popular services

RC MATTAR AWAPONGEZA DKT. SAMIA NA DKT. MWINYI, WANANCHI KASKAZINI UNGUJA WAJIVUNIA AMANI NA UTULIVU

 


Na: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, Mhe. Mattar Zahor Masoud, ametoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuchaguliwa na wananchi na kwa juhudi zao za kuimarisha amani na kuleta maendeleo nchini.

Mhe. Mattar ametoa pongezi hizo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari na watendaji mbalimbali wa serikali ofisini kwake Mkokotoni, Wilaya ya Kaskazini A, ambapo ameeleza kuwa hali ya usalama na utulivu kabla na baada ya uchaguzi imeendelea kuwa ya kuridhisha  jambo linaloleta faraja kwa wananchi wa mkoa huo na Zanzibar kwa ujumla.

Amesema wananchi, vyama vya siasa, viongozi wa dini, vyombo vya habari na vyombo vya ulinzi na usalama wameonyesha ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha amani, upendo na utulivu vinatawala katika kipindi chote cha kampeni hadi kukamilika kwa zoezi la uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Aidha, amewataka wananchi kuendeleza hali hiyo ya amani na mshikamano, na kuwaunga mkono viongozi wote waliochaguliwa katika majimbo yao pamoja na marais wa pande mbili za Muungano, ili Mkoa wa Kaskazini Unguja uendelee kusonga mbele katika nyanja zote za maendeleo kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wamesema uchaguzi wa mwaka huu umeandika historia mpya kutokana na hali ya amani na utulivu iliyotawala kabla na baada ya uchaguzi, tofauti na miaka iliyopita.

Wameeleza kuwa mshikamano baina ya wananchi na viongozi wa kitaifa umekuwa chachu ya maendeleo makubwa katika mkoa huo, hivyo wameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za viongozi wote nchini na kudumisha amani kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Kaskazini Unguja na Zanzibar kwa jumla.