Popular services

MNEC HABIBA AWASIHI WANACHI JIMBO LA AMANI KUICHAGUA CCM

 

NA FAUZIA MUSSA  

MRATIBU wa Kamati ya Kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Amani, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC), Habiba Ali Mohammed, amewasihi wananchi na wanachama wa chama hicho kukipa kura CCM katika uchaguzikuu ujao, akisisitiza kuwa ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuendeleza maendeleo ya kweli kwa Watanzania.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni ya nyumba kwa nyumba aliyoifanya kwa kushirikiana na kamati yake jimboni humo, MNEC Habiba alisema hakuna sababu ya wananchi kuchagua chama mbadala kwani CCM kina uzoefu, uongozi thabiti, na rekodi ya mafanikio yaliyothibitishwa.

 "Viongozi wetu si wageni kwenu. Wameshaongoza na mmeona matokeo ya kazi zao kupitia sekta mbalimbali. Msifanye mzaha katika uchaguzi huu, kwani mnapopoteza fursa ya kuwachagua, ni sawa na kupoteza nafasi ya maendeleo yenu wenyewe," alisisitiza MNEC Habiba.

MNEC Habiba  aliwaomba wananchi kuwachagua viongozi wakuu wa CCM wakiwemo Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, na Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Aidha, alisisitiza kuwa wagombea wa nafasi za ubunge na uwakilishi walioteuliwa na chama hicho wana uwezo wa kuwa kiunganishi kati ya wananchi na viongozi wa kitaifa katika kutafuta maendeleo ya majimbo yao.

Katika kuhakikisha ushiriki jumuishi wa wananchi wote, MNEC Habiba alieleza kuwa CCM kwa kushirikiana na mabalozi wa mashina, itahakikisha makundi maalum kama watu wenye ulemavu na wazee yanapata taarifa sahihi za sera na kuwezeshwa kushiriki uchaguzi kwa uhuru na haki.

"Chama kimejipanga kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma. Tunatambua umuhimu wa kila kura, na kila mwananchi anastahili kusikilizwa na kuwezeshwa," alisema.

MNEC Habiba pia aliwahimiza mabalozi wa mashina kuendelea kuwa daraja kati ya wananchi na viongozi wa serikali ili kusaidia kubaini changamoto mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati.

Hata hivyo, alikemea baadhi ya mabalozi ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo, hali inayosababisha viongozi kukosa taarifa sahihi kutoka kwa wananchi.

Kwa upande wao, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Jimbo la Amani waliahidi kushirikiana na serikali kuimarisha maendeleo jimboni humo, ikiwemo uimarishaji wa barabara za ndani na huduma muhimu nyingine za kijamii.

" Wakati huu  tuhamasishane kupiga kura na kuweka alama ya ndio katika kila mgombea wa CCM na baada tu ya kupata ridhaa zenu tutarudi tena kuja kusikiliza changamoto na kushirikiana na viongozi  wakuu kuzitafutia ufumbuzi" walisema

Naye Balozi wa Zone namba tano, Shina 25 – Amani, Saida Abdalla Ali, aliipongeza CCM kwa kuendesha kampeni ya nyumba kwa nyumba, akisema kuwa hatua hiyo imewafikia wapiga kura wengi kwa karibu na kuwapa nafasi ya kuelewa sera za chama.

"Tutahakikisha kila mpiga kura anafikiwa, anasikilizwa na anashiriki kikamilifu kupiga kura ifikapo Oktoba 25," alisema Saida.