Popular services

RC MATTAR AFANYA ZIARA YA KUSTUKIZA HOSPITALI YA KIVUNGE, ATOA WITO WA UDHIBITI WA MAENEO YA SKULI


Na: Nishan Khamis – Kaskazini “A”.
8-Oktoba 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, leo amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kivunge, Skuli ya Maandalizi na Msingi Kivoyoyo iliyopo Maafa, Nungwi, pamoja na Skuli ya Mlimani Matemwe, katika Wilaya ya Kaskazini “A”, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya ziara hiyo, Mhe. Mattar amesema lengo la ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Kivunge ni kukagua upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii, pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo ili kutafuta njia mbadala za kuboresha huduma kwa maendeleo ya hospitali na jamii kwa ujumla.

RC huyo amesema ameridhishwa na kiwango cha utoaji wa huduma, japokuwa bado kuna changamoto ndogo ndogo, hasa uhaba wa watumishi wa afya. Alibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi, tayari imetoa kibal na muda si mrefu tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Kwa upande wa ziara katika skuli hizo mbili, RC Mattar amesema lengo ni kudhibiti maeneo ya skuli kutokana na kuwepo kwa matukio ya uvamizi na wizi wa maeneo ya taasisi za elimu, jambo linaloweza kuathiri ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine ya skuli hapo baadaye.

Amewataka kamati za skuli, kamati za shehia, na jamii kwa ujumla kushirikiana kulinda maeneo hayo kwa maslahi ya maendeleo ya elimu katika maeneo yao na mkoa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Daktari Msaidizi wa Hospitali ya Wilaya ya Kivunge, Dk. Dhahey Rashid, amesema kuwa huduma za afya zinaendelea kutolewa kwa ubora licha ya changamoto zinazotokana na upungufu wa watumishi. Aliongeza kuwa wamewasilisha changamoto hizo wizarani kwa hatua zaidi, na akaomba ushirikiano wa uongozi wa mkoa katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, akibainisha kuwa malengo ya baadaye ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na kadi ya huduma za afya kwa mujibu wa sera ya serikali.

Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Mlimani Matemwe, Mariam Khamis Mwadin, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufika kusikiliza kilio chao, akieleza kuwa eneo la skuli limevamiwa na baadhi ya wananchi waliotaka kulipora. Amesema hawatarudi nyuma katika kulilinda eneo hilo kwa manufaa ya maendeleo ya elimu kwa watoto wa kijiji hicho.

Aidha, ameiomba serikali kusaidia ujenzi wa dahalia (hostel) kutokana na mazingira ya kijiji hicho kuwa ya utalii, jambo litakalosaidia wanafunzi kusoma kwa utulivu na kuendana na sera ya Uchumi wa Buluu.