Popular services

ELIMU YA KISHERIA YA NAPAC YALETA MABADILIKO DONGE MCHANGANI NA TAZARI


Na Nishan Khamis, Kaskazini Unguja

Wananchi wa Donge Mchangani na Tazari wameipongeza Taasisi ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC) kwa kuwafikia na kuwapatia elimu ya kisheria katika nyanja mbalimbali, pamoja na kusaidia kutatua changamoto za kisheria, hususan zile za kijamii, kupitia ufumbuzi wa kisheria wanaoupata.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya siku mbili ya NAPAC katika vijiji hivyo, Khamis Ali Haji kutoka Donge Mchangani na Salma Ibrahim kutoka Tazari Kilimani walisema hatua ya kufika vijijini, kusikiliza changamoto za wananchi na kutoa elimu ya kisheria ni jambo la kupongezwa. Wameishukuru NAPAC kwa jitihada zake za kusaidia jamii katika masuala ya kisheria yanayogusa maisha yao ya kila siku.


Walisema katika jamii yao bado kuna changamoto nyingi, hasa katika upatikanaji wa vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa, pamoja na uelewa mdogo kuhusu masuala ya kisheria katika kufuatilia haki zao. Hivyo, wametoa wito kwa NAPAC kuendelea na zoezi hilo muhimu kwa kuwa linachangia pakubwa kusaidia jamii, hasa zile za vijijini.

Kwa upande wake, Afisa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Wilaya ya Kaskazini A, Ali Haji Shamte, amewataka wanajamii kuhakikisha wanahakiki taarifa zao na kufuata taratibu za usajili wa matukio ya vizazi na vifo, ili kuhakikisha upatikanaji wa haki zao za kisheria na kuepuka usumbufu, udanganyifu na udhalilishaji unaoweza kujitokeza.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa mabalozi wazuri katika jamii zao, akieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imejikita katika kutoa huduma bora kwa wananchi wote nchini.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria wa NAPAC, Slima Husein Juma, alisema ziara hiyo ni miongoni mwa majukumu ya taasisi yao katika kusaidia jamii kupata uelewa wa masuala ya kisheria na kujua namna ya kudai haki zao kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa LEAP II ( Legal Empowerment and Access to justice Program chini ya ufadhili wa UNDP. Amewataka wananchi kushirikiana nao ili kufanikisha jitihada za kuisadia jamii ya Wilaya ya Kaskazini A na Zanzibar kwa ujumla.

Kwa ujumla, amesema elimu ya kisheria imeendelea kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, ikiwezesha wananchi kuelewa haki na wajibu wao, kupunguza migogoro, na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. NAPAC imesisitiza kuwa itaendelea kutoa huduma hizi kwa uwiano na ushirikiano wa karibu na wadau wa maendeleo.