NA FAUZIA MUSSA
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi,
amewaomba wanawake Waislamu nchini kuendeleza ibada ya dua kwa ajili ya
kuiombea nchi iendelee kubaki salama, yenye amani na utulivu, hasa katika
kipindi hiki kinapokaribia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza katika dua iloandaliwa na Kamati Maalum ya dua ya kitaifa ya wanawake kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, iliyofanyika katika Masjid
Mushawwal, Mwembe Shauri, Mama Mariam aliwashauri wanawake waislamu wa Zanzibar kuendeleza
juhudi hizo za dua na ibada ili nchi iendelee kuwa na amani ambayo ni msingi wa
ustawi wa jamii.
" Kwa uwezo
wa Mwenyezi Mungu na ushirikiano wa wananchi wote, uchaguzi ujao utakuwa
wa amani, wa haki na wa mafanikio kwa kila Mtanzania. Tunapaswa kumrudia Allah
Mtukufu kwa unyenyekevu, tumuombe aendelee kutuwekea neema ya Amani kwani endapo
amani itatoweka, wanawake na watoto ndio wahanga wakuu wa machafuko. Tumuombe
Mola wetu kwa unyenyekevu ili uchaguzi uje na upite kwa salama, bila chuki,
vurugu wala fitna.”
Aliongeza kuwa mafanikio na maendeleo ya Taifa
hayawezi kupatikana bila ya amani na utulivu, na kwa hivyo ni wajibu wa kila
Muislamu kushiriki katika maombi kwa makundi au mtu mmoja mmoja hata baada ya
uchaguzi, ili Zanzibar, Tanzania na ulimwengu mzima udumu katika hali ya amani.
“Wenzetu wanaoishi katika nchi zenye migogoro na
machafuko, hata mlo wa siku huwa ni mtihani. Hakuna kinachofanyika katika
mazingira ya taharuki. Amani ni msingi wa ustawi na maendeleo ya jamii,”
alisisitiza Mama Mariam.
Kiongozi wa dua hiyo, Maalim Sania, aliwashukuru
wanawake waislamu na waumini wengine kwa kujitokeza kwa wingi na kuungana na
viongozi wao katika ibada hiyo ya dua.
“Dua ni
silaha ya Muislamu. Tunapoomba kwa nia ya dhati, Allah hatushushi mikono
mitupu. Tunamuomba Atupitishe salama katika uchaguzi, atuwekee viongozi
waadilifu, wenye khofu ya Mwenyezi Mungu na walio tayari kuwatumikia wananchi
kwa moyo wa uaminifu,” alisema Maalim Sania.
Alieleza kuwa dua hizo ni ishara ya dhamira ya
Waislamu kuona taifa linapiga hatua kwa misingi ya amani, mshikamano na udugu
na kuongeza kuwa matumaini yao ni kuona
Allah anazidi kuwakinga wananchi na hofu, fitna na vurugu, na badala yake
kuzidisha mapenzi, umoja na mshikamano baina ya wananchi.
“Tumuombe Allah wakati wote, si tu kipindi cha
uchaguzi, bali kila siku. Hakika dua ni ibada na ni mlango wa faraja kwa
mwanadamu,” alisema maalim Sania
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya mama ya Wanawake Waislam wa Zanzibar, Hajjati Abla
Sultan Mahmoud, alisema lengo kuu la dua hiyo ni kumuomba Allah awape uwezo
wananchi kushiriki uchaguzi kwa salama, kwa uelewano na kwa moyo wa uzalendo.
Naye, Mjumbe wa Kamati ya Dua ya Kitaifa ya wanawake,
Khadija Ali Hassan, aliwakumbusha wanawake nafasi yao ya kipekee katika
kuhifadhi amani hasa kwa kulea vijana katika misingi ya dini na maadili mema.
“Wanawake tuendelee kuwa walinzi wa amani kupitia
malezi ya vijana wetu. Historia inatufundisha kuwa vijana wasiolelewa vyema,
ndio hutumiwa kama chombo cha kuvuruga utulivu wa taifa,” alisema Khadija.
Katika hafla hiyo, mamia ya wananchi kutoka mjini na
vijijini walihudhuria, wakiongozwa na Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi
mbalimbali wa serikali, taasisi za dini na madrasa za Zanzibar.