Na Nishan Khamis, Nungwi
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Nungwi leo wamefunga kampeni za mikutano ya hadhara kwa kishindo katika kiwanja cha mpira cha Hamburu, Nungwi, hafla iliyohudhuriwa na wanachama, wapenzi na wananchi mbalimbali wa jimbo hilo.
Mgeni rasmi, Mohamed Chombo, Mbunge mstaafu wa Jimbo la Magomeni, amewashukuru wananchi wa Nungwi kwa ushiriki wao mkubwa katika kipindi chote cha kampeni, akiwataka wasifanye makosa ifikapo Oktoba 29, bali waichague CCM ili kuendeleza uongozi wake serikalini. Alisisitiza kuwa maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa katika Jimbo la Nungwi ni matokeo ya juhudi za Serikali ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Akihitimisha kampeni hizo, Chombo amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kuelekea uchaguzi, akiwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kukipa ushindi wa kishindo chama hicho ili kiendelee kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wao, wagombea wa CCM wa nafasi mbalimbali katika Jimbo la Nungwi wamesema wamedhamiria kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM 2025–2030, kwa kusimamia miradi ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wanapata mafanikio zaidi katika sekta za kijamii na kiuchumi.
Aidha, wamewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuichagua CCM kwa kura nyingi za ndiyo, kwa maendeleo endelevu ya nchi, sambamba na kuwahakikishia kuwa usalama na amani vitaendelea kuwepo nchini katika kipindi chote cha uchaguzi.
Wananchi wa Nungwi wameishukuru Serikali ya CCM kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, afya na elimu, na wameomba ilani ijayo izingatie zaidi uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na ajira kwa vijana.
