Popular services

DKT MWINYI AMETUHESHIMISHA KIMAENDELEO-CCM JIMBO LA TUMBATU.

 

Na Nishan Khamis, Jimbo la Tumbatu

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Iddi Ali Ame, amesema kutokana na heshima kubwa ya Kisiwa cha Tumbatu na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, wananchi wa jimbo hilo na mkoa kwa ujumla wana kila sababu ya kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba na kuichagua CCM ili iendeleze maendeleo endelevu katika kisiwa hicho na Zanzibar kwa ujumla.

Mwenyekiti Iddi ameyasema hayo jana katika mwendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Tumbatu, wakati akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa fungu refu, Wilaya ya Kaskazini A , Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aidha, Mwenyekiti huyo amewasisitiza wananchi kuonesha umoja, ushirikiano na kudumisha amani —ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi  na kuwataka wasikubali kulubuniwa na watu wenye nia ovu za kupotosha dhamira njema ya maendeleo nchini.

Kwa upande wao, wagombea wa CCM wa jimbo hilo wamesema utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa vitendo umeimarisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, michezo, ajira, uchumi na ujenzi wa miundombinu. Wamesema ilani mpya ya CCM itenda kuimarisha zaidi na kuifungua kiuchumi kisiwa hicho hivyo kwa mikakati na mafanikio hayo wana kila  sababu za msingi kumuunga mkono Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi kubwa alizoonesha katika jimbo hilo, huku wakihimiza wananchi kuichagua CCM na kuunga mkono jitihada za marais wote wa Zanzibar na Tanzania Bara.

Aidha, wagombea hao wametumia nafasi hiyo kuhimiza utunzaji wa amani, upendo na ushirikiano, wakisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuichagua CCM ili iendelee kushika dola kwa kishindo na kuimarisha maendeleo zaidi.



Nao baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo wamesema wameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika jimbo hilo, hivyo wameomba kupitia ilani mpya ya CCM 2025-2030 ijikite katika kuwasaidia na kuwanyanyua wanawake kiuchumi kwa mikopo mingi siyo na riba pamoja na kuzidisha fursa za ajira kwa vijna na kuimarisha sekta ya michezo katika kisiwa hicho