Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kaskazini Unguja kimewataka vijana na vyama vyote vya siasa katika mkoa huo kuendelea kutunza amani na utulivu, sambamba na kuacha kulubuniwa na baadhi ya watu wenye nia mbaya ya kuvuruga amani iliyopo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Ndugu Iddi Ali Ame, wakati akizungumza katika mwendelezo wa kampeni za chama hicho katika jimbo la Mkwajuni, uliofanyika shehia ya Kibeni, wadi ya Kidombo, wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini Unguja.Amesema amani na utulivu ni tunu kubwa kwa taifa, hivyo CCM itaendelea kudumisha umoja, ushirikiano na kuhubiri amani na utulivu ndani ya mkoa huo na Zanzibar kwa ujumla. Aidha, amewataka vijana wa shehia ya Kibeni, mkoa mzima wa Kaskazini Unguja pamoja na vyama vyote vya siasa kuhakikisha wanailinda tunu hiyo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya nchi.
Mwenyekiti huyo amewanasihi vijana na jamii kwa ujumla kufuata kanuni na sheria za Tume ya Uchaguzi, na ifikapo siku ya uchaguzi kujitokeza kwa wingi kuwachagua viongozi wa CCM kwa maendeleo zaidi ya nchi. Amesema kufanya hivyo kutaendelea kukiimarisha chama hicho kushika dola kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wao, wagombea wa CCM katika jimbo hilo wamesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025 umefikia zaidi ya asilimia mia moja kutokana na usimamizi makini wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi. Wamesema mafanikio hayo ni sababu tosha ya kuendelea kuiweka CCM madarakani ifikapo Oktoba 29 mwaka huu kwa kuwapa kura za ndiyo viongozi wote wa chama hicho.
Aidha, wamesema watahakikisha wanashughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Kibeni na jimbo zima la Mkwajuni, ikiwemo upatikanaji wa huduma bora za maji na miundombinu ya barabara.
Wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo wamepongeza uongozi wa chama kwa usimamizi wa vitendo katika utekelezaji wa Ilani. Hata hivyo, wamebainisha changamoto za ukosefu wa maji safi na ubovu wa barabara katika wadi hiyo, wakiiomba serikali kuzishughulikia kwa haraka.
Sambamba na hayo, wamemuomba Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kuendelea kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa vijana na wanawake ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi. Wameahidi kuwa ifikapo Oktoba 29, kura zote za “ndiyo” watapeleka kwa CCM kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
