Popular services

CCM YASISITIZA WATUMBATU WASIKUBALI KULUBUNIWA, YAHIMIZA AMANI NA KUICHAGUA CCM OKTOBA 29


Na Nishan Khamis, Tumbatu

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Iddi Ali Ame, amesema kutokana na heshima kubwa ya Kisiwa cha Tumbatu na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, wananchi wa jimbo hilo na mkoa kwa ujumla wana kila sababu ya kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura tarehe 29 Oktoba na kuichagua CCM ili iendeleze maendeleo endelevu katika kisiwa hicho na Zanzibar kwa ujumla.

Mwenyekiti Iddi ameyasema hayo jana katika mwendelezo wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Tumbatu, wakati akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Jongowe, Wilaya Ndogo ya Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya usimamizi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, kupitia utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM, ni kielelezo cha uongozi bora na utendaji makini wa chama hicho. Ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kumuunga mkono kwa kuhakikisha kwamba ifikapo Oktoba 29 wanajitokeza mapema kwenda kupiga kura na kuichagua CCM kwa kura nyingi za ndiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo amewasisitiza wananchi kuonesha umoja, ushirikiano na kudumisha amani — ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi — na kuwataka wasikubali kulubuniwa na watu wenye nia ovu za kupotosha dhamira njema ya maendeleo nchini.

Kwa upande wao, wagombea wa CCM wa jimbo hilo wamesema utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa vitendo umeimarisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, michezo, ajira, uchumi na ujenzi wa miundombinu. Wamesema mafanikio hayo yanatoa sababu za msingi kumuunga mkono Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi kubwa alizoonesha katika jimbo hilo, huku wakihimiza wananchi kuichagua CCM na kuunga mkono jitihada za marais wote wa Zanzibar na Tanzania Bara.

Aidha, wagombea hao wametumia nafasi hiyo kuhimiza utunzaji wa amani, upendo na ushirikiano, wakisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuichagua CCM ili iendelee kushika dola kwa kishindo na kuimarisha maendeleo zaidi.

Nae,Mbunge mteule wa viti maalumu UWT mkoa wa Kaskazini Unguja Shadya Haji Omar, amewahimiza vijana wa jimbo la Tumbatu na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa kutunza na kuhubiri amani kabla na baada ya uchaguzi na wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29 kwa kuichagua CCM kwa kura za ndio.

Nao baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo wamesema wameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika jimbo hilo, wakibainisha kuwa “Tumbatu ya miaka mitano ya uongozi wa Dk. Hussein Mwinyi ni Tumbatu ya maendeleo kwa kila nyanja.”

Wameahidi kuonesha hisani yao kupitia kura nyingi za ndiyo kwa Chama Cha Mapinduzi ifikapo Oktoba 29.