Na: Nishan Khamis – Mkwajuni
Tarehe: 11 Oktoba 2025
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imewahimiza walimu wakuu mkoa wa Kaskazini Unguja kuhakikisha wanashirikiana ipasavyo katika kukuza ufaulu wa wanafunzi kwa manufaa ya maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Utawala wa Wizara hiyo, Dkt. Khalid Masoud Wazir, alipokuwa akizungumza na maafisa elimu wa mkoa huo pamoja na walimu wakuu wa shule za maandalizi, msingi na sekondari katika kikao kilichofanyika Skuli ya Sekondari Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A.
Dkt. Khalid amesema bado kuna changamoto kwa baadhi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na kuingia sekondari kutokujua kusoma na kuandika, jambo linalohitaji juhudi za pamoja kutoka kwa walimu ili kutatua changamoto hiyo. Aliongeza kuwa serikali imelitambua tatizo hilo na inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha maendeleo ya elimu nchini.
Aidha, amewataka walimu kusimamia matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wanafunzi na kuhakikisha miongozo ya wizara inafuatwa ipasavyo. Vilevile, alimpongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa hatua kubwa alizochukua katika kuimarisha sekta ya elimu, akisema walimu wana kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizo katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Dkt. Khalid pia amewataka walimu kuwa mabalozi wa amani na utulivu katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, akisisitiza kuwa itikadi bora ni maendeleo na hivyo ni wajibu wa walimu kuhamasisha amani na mshikamano nchini.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bi. Subira Abdalla Vuai, alimshukuru Dkt. Khalid kwa mwongozo alioutoa na akaahidi kuwa yeye pamoja na maafisa wake wa wilaya watatekeleza maagizo yote kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu katika mkoa huo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya walimu, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Potoa, Suleiman Mtwana Khamis, amempongeza Naibu Katibu kwa ziara yake yenye tija na akaahidi kuwa walimu wataendelea kudumisha amani, utulivu na ushirikiano, sambamba na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura kumuunga mkono Rais Dkt. Hussein Mwinyi ili aendelee kuimarisha maendeleo ya elimu Zanzibar.
Jumla ya walimu 250 kutoka skuli za maandalizi, msingi na sekondari mkoa wa Kaskazini Unguja walihudhuria katika kikao hicho..

