Nishan khamis-Nungwi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Amin Salmin Amour, ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi kupitia Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Nungwi, leo amezindua kampeni ya Amka Nungwi Kumekucha yenye lengo la kuendelea kuhamasisha amani na utulivu, kuwatembelea mabalozi, upachikaji wa bendera pamoja na kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa katika jimbo hilo.
Amesema jimbo hilo lipo salama na wananchi wana kila sababu ya kutumia haki yao ya kikatiba ifikapo Oktoba 29 kwa kujitokeza kwa wingi kwenda kuichagua CCM iendelee kuwa madarakani kwa kuendeleza maendeleo zaidi nchini.
Aidha, amesema jimbo hilo lina kila sababu ya kupata ushindi ifikapo Oktoba 29 na kuacha kulubuniwa na baadhi ya wanasiasa wenye nia mbaya ya uvunjifu wa amani nchini jambo ambalo vyombo vya ulinzi na usalama vipo makini katika kuendelea kulinda amani kabla na baada ya uchaguzi.
Amewahakikishia wananchi wa Nungwi kuwa, pamoja na changamoto ndogo ndogo hasa ya maji, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni serikali ya utekelezaji wa vitendo, ambapo tatizo hilo tayari limeanza kushughulikiwa. Hivyo amewaomba wananchi wawe na uvumilivu kipindi hiki kifupi na waendelee kuunga mkono jitihada zote za maendeleo zinazotekelezwa katika jimbo hilo.
Wakizungumza katika ziara hiyo, Mgombea Ubunge na Uwakilishi kupitia CCM Jimbo la Nungwi, wamesema ziara hiyo ina umuhimu mkubwa hasa katika kufanya tathmini, kwani mabalozi ni watu wenye nafasi muhimu katika kukipatia ushindi chama. Wameeleza kuwa ziara hiyo inaendelea kuhamasisha amani na kuwahimiza wananchi kujitokeza tarehe 29 siku ya uchaguzi na kuichagua CCM kwa kishindo kwa ajili ya maendeleo zaidi.
Nao wanachama wa chama hicho na baadhi ya mabalozi wamesema wamefurahishwa na ziara hiyo kwani imewahamasisha wanachama na wananchi kwa ujumla kuendelea kutunza amani na kujitokeza siku ya kupiga kura. Wamesema wamejipanga na wana kila sababu ya ushindi, hivyo wametoa wito kwa vijana, wazee na wananchi kwa ujumla wa jimbo hilo kujitokeza Oktoba 29 kwenda kuichagua CCM kwa kura nyingi za “ndiyo” kwa maendeleo ya Nungwi na Zanzibar kwa ujumla.
Ziara hiyo ni ya siku tatu, ambapo jumla ya mabalozi 99 wanatarajiwa kutembelewa na kupachikiwa bendera ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kichama katika jimbo hilo.



