22 Oktoba 2025
Jumuiya na Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) nchini zimetakiwa kuzingatia misingi, sheria na taratibu za uendeshaji wao hususani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuepuka kujiingiza katika masuala ya kisiasa na badala yake kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya jamii.
Akifungua mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Tumekuja, Wilaya ya Mjini Unguja, Mrajisi wa Asasi zisizo za Kiserikali Zanzibar Ahmed Khalid Abdulla amesema kupitia Sheria Na. 6 ya mwaka 1995 na Sera ya mwaka 2009 inazitambua jumuiya na asasi za kiraia kama wadau muhimu wa maendeleo, hivyo ni wajibu wao kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria, taratibu, mila na silka za Zanzibar.
Aidha amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwapatia washiriki taaluma kuhusu wajibu, malengo na mtazamo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa asasi hizo pamoja na kuhimiza umuhimu wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa shughuli zao kwa Ofisi ya Mrajisi, ili kuwezesha Serikali kufuatilia maendeleo na changamoto zinazowakabili.
Aidha, viongozi wa jumuiya wametakiwa kuepuka kuendesha shughuli zao kwa misingi ya kisiasa, kuwa makini na uingizaji wa fedha kinyume na taratibu za kisheria na badala yake kuendelea kutekeleza sera za Serikali sambamba na kuheshimu mila, silka na utamaduni wa Zanzibar.
Mrajisi Abdulla alihimiza asasi hizo kuimarisha umoja na ushirikiano, kuepuka migogoro, na kuhakikisha zinasaidia wananchi kwa vitendo badala ya malumbano yasiyo na tija. Pia amewataka viongozi wa jumuiya kuwa mabalozi wa amani na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kutimiza takwa la kikatiba kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Safina Masoud Khamis akiwasilisha mada katika mafunzo hayo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia aina za usajili na taratibu za kisheria ambapo taasisi zote lazima ziwe za hiari, zisijihusishe na siasa, na zielekeze nguvu katika kutatua changamoto za jamii.
Washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Ofisi ya Mrajisi wa NGOs Zanzibar kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla huku wakiahidi kuwa mabalozi wa amani, umoja na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
