Na: Nishan Khamis – Nungwi
11 Oktoba, 2025
Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) katika wadi ya Bandakuu, Nungwi, kimeahidi kwamba endapo kitapata ridhaa ya wananchi kuchaguliwa diwani, kita hakikisha kinasimamia utatuzi wa changamoto zote zinazowakabili wakazi wa kijiji hicho kwa lengo la kujenga ustawi wa jamii ya Nungwi.
Ahadi hiyo imetolewa na mgombea udiwani wa wadi hiyo kupitia tiketi ya CHAUMMA, Ndugu Sharif Mwalimu Juma, wakati akijinadi na kuomba kura katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha tawi la ACT-Wazalendo, Nungwi.
Amesema kijiji hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maji safi, migogoro ya ardhi, upatikanaji wa mikopo kwa vijana, wavuvi na wanawake, pamoja na ukosefu wa ajira. Amesisitiza kuwa, endapo atachaguliwa, atahakikisha anasimamia kikamilifu utatuzi wa changamoto hizo ili kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Nungwi.
Aidha, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kumchagua, akiahidi kwamba “wakimchagua, watakula ubwabwa kwa wingi.” Amehimiza pia utunzaji wa amani na utulivu, huku akiomba jeshi la polisi kuendelea kulinda usalama wa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA Zanzibar, Mohamed Husein, amemuombea kura mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Mwalimu Salum, akiwataka wananchi wa Nungwi, vijana na vyama vya upinzani kumpa kura, akisema ni kijana mwenye maono ya maendeleo ya taifa.
Zaidi ya watu 70 walihudhuria mkutano huo, ambapo baadhi ya wananchi walisema wamesikiliza kwa makini sera za chama hicho na kuvutiwa nazo, hasa sera yake ya “ubwabwa” pamoja na dhamira ya chama hicho kuendeleza ujumuishi na usawa kwa wananchi wote nchini.
