Na: Nishan Khamis – Kaskazini Unguja
Katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu, mbinu ya kampeni za nyumba kwa nyumba imeendelea kuwa moja ya nyenzo muhimu inayotumiwa na wagombea mbalimbali, hususani wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi.
Mbinu hii, licha ya kuhitaji muda, nguvu, na uvumilivu, imeonekana kuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea wanawake uaminifu wa kisiasa na kuimarisha ushiriki wao katika siasa za Zanzibar.
Mwaduwa Ali Khamis, mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Bumbwini, amesema changamoto kubwa anayokutana nayo ni mitazamo hasi ya kijinsia, ukosefu wa rasilimali kama usafiri, fedha, na wakati mwingine hata unyanyasaji wa kijinsia kutokana na kuonekana kwamba mwanamke anayejihusisha na siasa ni muhuni.
“Unapopita nyumba kwa nyumba, si kila mtu anakukaribisha kwa furaha , wapo wanaokuona kama unavunja mipaka ya kijinsia au kama uhuni, lakini ukiwa na uthubutu na uaminifu, unapata nafasi ya kueleweka na kufanya ushawishi mkubwa wa kueleweka,” amesema Mwaduwa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA-ZANZIBAR) Zanzibar Agosti 20, 2025, imeeleza kuwa jumla ya wanawake 13 nchini kutoka vyama mbalimbali vya siasa wamegombea nafasi ya urais na umakamu wa rais, idadi sawa na asilimia 36 kati ya wagombea wote waliochukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Hii ni idadi iliyoonyesha ongezeko ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo wanawake walikuwa 7 pekee, sawa na asilimia 23.3.
Ripoti ya UN Women ya mwaka 2022 imebainisha kuwa mbinu za kampeni za nyumba kwa nyumba ni kati ya mikakati inayoongeza uaminifu wa wananchi kwa wagombea wanawake, hasa katika jamii zenye mitazamo ya kijinsia inayowabagua wanawake. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanawake wanaotumia mbinu hii hufanikiwa kujenga uhusiano wa karibu na wapiga kura kwa asilimia 35 zaidi kuliko wale wanaotegemea mikutano mikubwa pekee.
Nyange Kher Ali, mwanadiplomasia kijana kutoka kijiji cha Gamba na mgombea udiwani wa wadi ya Gamba kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema mbinu ya nyumba kwa nyumba imekuwa msaada mkubwa kwao kujenga uhusiano wa karibu na wananchi.
“Unapozungumza na mtu uso kwa uso, anakusikiliza, anakuelewa, na mara nyingi anakupa imani yake. Hii mbinu ni bora sana hata mimi natumia katika kampeni zangu,ni vyema kwa wanawake viongozi kipindi hichi wakazidi kuitumia mbinu hii,” ameeleza Nyange.
Kwa mujibu wa Mchambuzi wa Siasa, Selemani Makwita kutoka Action for Democratic Governance (ADG) Dar es Salaam, amesema kampeni za nyumba kwa nyumba zinatoa nafasi kwa wanawake kujenga imani ya moja kwa moja na wapiga kura, tofauti na mikutano mikubwa ya kisiasa ambayo mara nyingi haina mawasiliano ya karibu.
“Mbinu hii inaleta ushawishi wa kipekee kwa wanawake, hasa wale wanaotoka katika jamii zinazowatizama kama dhaifu. Hii ni njia ya kujenga uhalisia wa uongozi wao kwa vitendo,” amesema Makwita.
Ameshauri kuwa ili mbinu hii iendelee kuwa na mafanikio, ni muhimu wanawake wakawezeshwa kielimu na kifedha, na chama chochote kinachowaunga mkono kiweke mkazo katika kuwapatia mafunzo ya mawasiliano ya kisiasa.
Kwa upande wa viongozi wa mitaa na wanajamii, mtazamo kuhusu wanawake wanaofanya kampeni za nyumba kwa nyumba umeanza kubadilika taratibu,Sheha wa Shehia ya Mkwajuni, Jumbe Iddi Jumbe, amesema zamani baadhi ya wananchi walionekana kushangazwa kuona wanawake wakitembea nyumba kwa nyumba wakisaka kura hasa nyakati za usiku, lakini sasa jamii imeanza kuelewa umuhimu wa mbinu hiyo.
“Watu wameanza kuona si ajabu tena, na ni njia bora kwa mwanamke kuwa kwenye kampeni za nyumba kwa nyumba kwani wanawake hawa wanaonyesha mfano wa ujasiri, kujituma, na kuonesha muamko wao katika siasa na uongozi,” amesema Sheha Jumbe.
Baadhi ya wakazi wa shehia pia wanakiri kuwa kampeni hizo zimewasaidia kufahamu vyema sera za wagombea.“Mimi binafsi siendi kwenye mikutano ya hadhara, lakini naona wanawake na wanaume wanakuja kueleza sera zao na kuomba kura, na huwa navutiwa na ushawishi wao,mimi pia nawaunga mkono wanawake wenzangu,” amesema Tano Othman, mkaazi wa Shehia ya Kivunge.
Baadhi ya wanawake waliofanikiwa kisiasa kupitia kampeni za nyumba kwa nyumba wanasema siri yao ni kujenga uhusiano wa karibu na wananchi,Siti Ali Makame, aliyekuwa diwani wa wadi ya Banda Kuu Nungwi, amesema “Nilijifunza kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza,nilijua matatizo yao, nikawa sehemu ya suluhisho,hiyo ndiyo iliyonivusha kwa sera na ushawishi mkubwa kwa wanawake na vijana katika kampeni za nyumba kwa nyumba.” amesema Siti.
Kwa upande wa mwanaharakati wa maswala ya wanawake Farihia Abdalla Juma, Katibu wa Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja, amesema kampeni za nyumba kwa nyumba zinachukuliwa kama hatua muhimu ya kupaza sauti ya wanawake katika siasa, kwani zinavunja vizuizi vya kijamii vilivyowafanya wanawake wabaki nyuma kwa muda mrefu.
“Ni mbinu mzuri sana kutumia kwani unavyomfata mtu kwa ustaarabu ni rahisi kukuelewa haraka zaidi. Kwa upande wangu, nawahamasisha wanawake wenzangu kutumia mbinu hii,” amesema Farihia.

