Popular services

NAPAC YASAMBAZA ELIMU YA MPIGA KURA SHEHIA YA GAMBA, WAHAMASISHA WATU WENYE ULEMAVU KUJITOKEZA SIKU YA UCHAGUZI


Na Nishan Khamis – Gamba

Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Kaskazini A (NAPAC) leo imetoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi wa Shehia ya Gamba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa tamko la kisheria la Uchaguzi Na. 4 la mwaka 2018 na Kanuni za Uchaguzi kifungu cha 144(1). Lengo la shughuli hiyo ni kuielimisha jamii juu ya utambuzi wa demokrasia, amani, na ushiriki katika mchakato wa uchaguzi nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Msaidizi wa Sheria wa Wilaya hiyo, Salma Ibrahim Juma, alisema kuwa suala la uchaguzi ni haki ya kidemokrasia, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa jamii kuchagua viongozi wanaowataka kwa misingi ya amani na utulivu, kwani hayo ni mambo ya msingi katika kuimarisha umoja wa kitaifa. Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwaelimisha vijana juu ya umuhimu wa kudumisha amani hasa katika kipindi cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Katibu wa Watu Wenye Ulemavu wa Wilaya hiyo, ambaye pia ni Msaidizi wa Sheria, Ulaya Khamis Juma, amehimiza jamii kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa ipasavyo katika mchakato wa uchaguzi, akisisitiza ushiriki wao wa moja kwa moja ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.

Naye Sheha wa Shehia ya Gamba, Khamis Ame Khamis, alipofunga kikao hicho, aliipongeza NAPAC kwa juhudi zao za kutoa elimu hiyo muhimu kwa wananchi. Amesema ataendeleza elimu hiyo katika jamii kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.