Na, Nishan Khamis, Fukuchani
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Nungwi, Ali Habib Mtwana, amesema ujenzi wa soko la kisasa la samaki katika Shehia ya Fukuchani utafungua fursa za kiuchumi na kibiashara katika jimbo hilo na Zanzibar kwa ujumla.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini A, amesema CCM inaendelea kutekeleza Ilani yake kwa vitendo katika jimbo hilo.
Ameeleza kuwa miradi mikubwa ikiwemo ya maji, barabara, ujenzi wa kituo cha afya cha kisasa pamoja na soko hilo la samaki ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Aidha, ametoa wito kwa jamii kuendelea kudumisha amani na utulivu, pamoja na kuunga mkono juhudi za viongozi katika kuleta maendeleo. Amesema uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na viongozi wa jimbo hilo, ni hatua muhimu katika kuimarisha maendeleo ya eneo hilo.
Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Wavuvi wa Shehia ya Fukuchani, Sumai Ali Makame, ameishukuru Serikali na viongozi wa jimbo kwa ujenzi wa soko hilo.
Amesema hapo awali wavuvi na wafanyabiashara walikabiliwa na changamoto ya kukosa soko bora na lenye mazingira rafiki kwa shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa soko hilo kutachochea ukuaji wa biashara katika eneo hilo na Zanzibar kwa ujumla, kutokana na kuimarika kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanyika katika shehia hiyo.

