Popular services

MHE. AYOUB ASHIRIKIANA NA FAROUK KUTOKA UINGEREZA NA SAMIR KATIKA UTOAJI WA SADAKA YA IFTAR KWA WAZEE WA JIMBO LA CHAANI.


Na, Nishan Khamis – Chaani
Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud kwa kushirikiana na Bwana Farouk Sumra kutoka nchini Uingereza sambamba na Samir Ayoub, mkaazi wa Zanzibar, leo wamewafariji wazee wa jimbo la Chaani kwa kuwapatia sadaka ya iftar ili kuwasaidia kujikimu katika mfungo mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Samir Ayoub pamoja na Farouk Sumra wamesema kuwa kutokana na ushirikiano mzuri waliokuwa nao na Mbunge huyo, wameona umuhimu wa kuwapatia wazee wa jimbo hilo sadaka, japo kwa kiwango kidogo, ili waweze kujikimu katika kipindi hiki cha Ramadhan.

Wamesema jimbo hilo limebahatika kuwa na kiongozi mbunifu mwenye mahusiano mazuri na wadau mbalimbali, jambo linalowapa moyo wa kushirikiana katika kusaidia maendeleo ya wananchi. Aidha, waliwashukuru wananchi kwa muitikio wao mkubwa na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika utoaji wa sadaka mbalimbali.

Vilevile, wametoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi kwa uongozi wao unaoleta maendeleo, huku wakihimiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.

Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Khamis, amesema utoaji wa sadaka hiyo ni sehemu ya mikakati ya viongozi wa jimbo hilo katika kuwatumikia wananchi wao katika nyanja mbalimbali. Amewashukuru wadau waliochangia sadaka hiyo na kuahidi kuwa zoezi la utoaji wa misaada litaendelea kwa makundi tofauti ndani ya jimbo hilo.

Nao wazee waliopatiwa sadaka hiyo wametoa shukrani zao za dhati kwa msaada huo, wakisema ni muhimu hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan. Wamewaomba viongozi na wadau kuendelea kuwasaidia katika mahitaji yao ya kila siku.

wazee zaidi ya 50 walipatiwa sadaka iyo vikiwemo sukari,unga ngano,tambi, mchele mafuta pamoja na tende ili wajikimu katika kipindi hiki cha Ramadhan.