Popular services

KITUO CHA POLISI CHAANI LUNGALUNGA KUJENGWA UPYA, MHE. AYOUB ATOA MILIONI 9; VIJANA WA HAMASA WAPEWA LAKI 5.

 

Na Nishan Khamis, Chaani
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, leo amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Polisi Kisiwa cha Tumbatu pamoja na nyumba za askari polisi. Aidha, alitembelea Kituo Kidogo cha Polisi kilichopo Chaani Lungalunga kwa lengo la kuimarisha mazingira rafiki kwa Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa wananchi.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo na wananchi wa Jimbo la Chaani pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Ayoub amesema kuwa hali ya Kituo cha Polisi Lungalunga hairidhishi katika utoaji wa huduma kwa wananchi kutokana na uchakavu wake.

Amesema Serikali ya Tanzania ina mpango wa kujenga zaidi ya vituo vya polisi 3,900 nchini kote, na kituo cha Lungalunga ni miongoni mwa vituo vitakavyojengwa upya. Aidha, ameliagiza Jeshi la Polisi kuzingatia ujenzi huo na kuhakikisha kuwa pindi ujenzi utakapoanza, mafundi na vibarua watatoka katika Jimbo la Chaani ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa eneo hilo.

Mhe. Ayoub amesema kuwa kutokana na umuhimu wa huduma bora za ulinzi na usalama, ni lazima kijengwe kituo chenye hadhi kitakachokidhi mahitaji ya wananchi. Katika kuonesha dhamira hiyo, amekabidhi shilingi milioni tisa na kulitaka Jeshi la Polisi kuchangia shilingi milioni moja ili kukamilisha fidia ya shilingi milioni kumi kwa wananchi waliotoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Mwandamizi wa Polisi Benedict Mapujila, amesema uchakavu wa kituo hicho umekuwa ukisababisha askari kufanya kazi katika mazingira magumu, jambo linaloathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Khamis, akizungumza kwa niaba ya wananchi, alimshukuru Naibu Waziri kwa ziara hiyo na kueleza kuwa imeleta matumaini mapya kwa wananchi katika juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama kupitia ujenzi upya wa kituo hicho.

Mbali na hilo, Mhe. Ayoub alitoa shilingi laki tano kwa vijana wa hamasa wa jimbo hilo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kimichezo.