Na Nishan Khamis, Gamba
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ngazi ya Wilaya na Taifa, Mabaraza ya Vijana, Ame Haji Vuai , amewahakikishia vijana kuwa uchaguzi utakuwa wa haki, uwazi na uwajibikaji.Amesema hayo leo wakati akizungumza katika ziara yake ya kuwatembelea maafisa wa usimamizi wa uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini A na Kaskazini B Unguja, ambapo pia alipata fursa ya kukagua maandalizi ya zoezi la uchaguzi.
Katika ziara hiyo, amepongeza mwamko mkubwa wa vijana katika uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, akieleza kuwa hali hiyo inaonesha utayari na hamasa ya vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.
Ameeleza kuwa kamati ya uchaguzi imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza amani na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi.
Nae, mjumbe wa Kamati ya Wilaya ya Kaskazini A, Khamis Rashid Khamis, wamemhakikishia mwenyekiti huyo kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji ili kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.
