Na Nishan Khamis,
Mkwajuni.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Jimbo la Mkwajuni, kwa kushirikiana na Diwani wa Wadi ya Kidombo pamoja na Diwani wa Kuteuliwa wa Wilaya ya Kaskazini A, Jabu Hamdu Makame, leo wameshiriki katika mazoezi ya pamoja na vijana wa Kundi la Hamasa la Jimbo la Mkwajuni.
Akizungumza mara baada ya mazoezi hayo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa jimbo hilo, Changariro, ametoa pongezi za dhati kwa vijana hao kwa kuendeleza tabia ya kufanya mazoezi yenye tija. Sambamba na hilo, amewapongeza madiwani hao wawili kwa ushiriki wao na kuwa pamoja na vijana hao, akieleza kuwa ni jambo jema linalojenga ushirikiano mzuri kati ya viongozi na vijana katika kupeleka mbele maendeleo ya wadi na jimbo kwa ujumla.
Aidha, amewanasihi vijana hao kuzingatia nidhamu, heshima na weledi ndani ya kundi lao, pamoja na kuepuka vishawishi vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na kudhoofisha maendeleo ya kundi hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa Unju amewahakikishia vijana kuwa ataendelea kushirikiana nao kwa hali na mali katika harakati zao zote kwa ajili ya maendeleo ya wadi na jimbo kwa ujumla.
Naye, Diwani Jabu Hamdu Makame, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, amesema mazoezi ni jambo la msingi, akieleza kuwa hata Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akihimiza wananchi kushiriki mazoezi. Amesema kuendelea kwa vijana hao kufanya mazoezi ni kuunga mkono juhudi za Dkt. Mwinyi katika kuimarisha afya ya jamii.
Ameendelea kuwasisitiza vijana hao kuendeleza mazoezi sambamba na kutunza amani na utulivu uliopo nchini. Katika kuhamasisha michezo, Mhe. Jabu Hamdu Makame aliwakabidhi vijana hao fedha taslim ili kuwasaidia katika harakati zao za michezo.
Nao vijana wamesema wamefurahishwa na ushiriki wa viongozi hao katika mazoezi, wakieleza kuwa hatua hiyo imetoa taswira njema ya ushirikiano kati yao na viongozi katika masuala ya michezo na shughuli nyingine za kijamii kwa maendeleo yao na Jimbo la Mkwajuni kwa ujumla.

