Na Nishan Khamis, Kivunge
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dkt. Riziki Pembe Juma, amefanya ziara maalum katika Hospitali ya Kivunge kwa lengo la kuwatembelea wanawake na watoto, kujionea hali ya huduma za afya wanazopata pamoja na kutoa msaada wa sabuni, unga wa lishe na mashuka pamoja na vitu mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya hospitalini .
Dkt. Riziki amesema kuwa ziara hiyo ni miongoni mwa mikakati yake ya kuendelea kuwaunga mkono wanawake na watoto katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, sambamba na kuwashukuru wanawake kwa imani waliyoonesha kwake kwa kumchagua kuwa Mwakilishi wao kupitia viti maalum. Ameeleza kuwa ni wajibu wake kushirikiana na wanawake kwa hali zote kwa maslahi ya maendeleo yao, na kuahidi kuendelea kutoa msaada unaolenga kuboresha ustawi wa wanawake na watoto.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwasaidia wanawake katika masuala ya usafi na afya, akieleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii. Hivyo, ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.
Vilevile, amewashukuru wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, na kuwapongeza Madiwani pamoja na wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa mshikamano na ushirikiano wao katika kuendeleza agenda ya afya na ustawi wa wanawake na watoto. Pia, amekishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyoonesha kwake, akiahidi kuendelea kuwatumikia wanawake na watoto kwa uadilifu na kujitolea.
Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya Kivunge, Leonard Godwin Mgana, ametoa pongezi za dhati kwa Dkt. Riziki Pembe Juma, akieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Dkt. Hussein Mwinyi, na kwamba una manufaa makubwa kwa wanawake na watoto wanaopata huduma katika hospitali hiyo. Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kusaidia mahitaji mbalimbali ya hospitali hiyo.
Naye, Mjumbe wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kaskazini “A”, ambaye pia ni Diwani wa Kuteuliwa Jimbo la Kijini, Chembe Khamis Sheha, ametoa pongezi kwa Dkt. Riziki, akisema amekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia changamoto za wanawake na watoto katika wilaya hiyo. Ameongeza kuwa wanawake wa mkoa huo wataendelea kumuunga mkono katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo.
