Popular services

MHE AYOUB AWAGUSA WANANCHI WA CHAANI KWA SADAKA YA IFTAR, ZAIDI YA WATU 150 WANUFAIKA.

 

Na Nishan Khamis, Chaani
Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mheshimiwa Ayoub Mohammed Mahmoud, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Tanzania, ameanza kutoa sadaka ya iftar kwa wakaazi wa jimbo lake ikiwa ni sehemu ya kuendeleza ahadi zake za kuwatumikia wananchi katika harakati mbalimbali za kimaendeleo.

Sadaka hiyo ilikabidhiwa katika hafla maalum ambapo Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Khamis, alimwakilisha Mheshimiwa Mbunge. Akizungumza kwa niaba yake, diwani huyo alisema kuwa utoaji wa sadaka hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano wa viongozi wa jimbo hilo katika kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, kwani wote ni wamoja.

Ameeleza kuwa zoezi hilo ni mwanzo tu, na kwamba wataendelea kutoa misaada kama hiyo kwa mashirikiano ya viongozi wote wa jimbo hilo. Aidha, ametoa wito kwa wadau na wahisani mbalimbali kujitokeza kushirikiana katika kuleta misaada na kuchangia juhudi za maendeleo ya Jimbo la Chaani.

Vyakula vilivyotolewa ni pamoja na maharage, mchele, unga wa ngano, sukari na mafuta ya kupikia, ambapo zaidi ya wananchi 150 walinufaika na msaada huo.

Kwa upande wao, wananchi waliopokea sadaka hiyo wametoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Mbunge na kumuombea dua ili aendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku akiendelea kuwaletea maendeleo zaidi.