Na Nishan Khamis, Nungwi
Zaidi ya wananchi 500 wa Nungwi wamepatiwa sadaka ya chakula kwa ajili ya iftar na daku kutoka Taasisi ya Sister Island, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Sadaka hiyo imetolewa kwa wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika Skuli ya Sister Island iliyopo Nungwi pamoja na wananchi wengine wenye uhitaji kutoka maeneo mbalimbali ya Nungwi, ikiwa ni jitihada za kuwawezesha kupata futari na daku katika mwezi huu mtukufu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Nungwi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sister Island, Francesca Michael, amesema taasisi hiyo ni sehemu ya jamii ya Nungwi na inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wake. Ameeleza kuwa utoaji wa sadaka hiyo ni muendelezo wa juhudi za taasisi katika kusaidia jamii na kuchangia maendeleo.
Kwa upande wake, Mhasibu wa taasisi hiyo, Haji Moh’d Ali, amesema jumla ya kilo 2,500 za mchele na kilo 1,500 za njugu zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya 500 wa Nungwi. Amesema huo ni utaratibu wa kawaida wa taasisi kila unapofika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, sambamba na kuendelea kusaidia jamii hata katika miezi mingine.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuwaletea wananchi maendeleo, huku akisisitiza ushirikiano kati ya taasisi, serikali na jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Nungwi wamesema taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya eneo hilo, hasa kwa watoto, wanawake na vijana. Wametoa pongezi na shukrani za dhati kwa uongozi wa taasisi hiyo kwa moyo wa kujitolea kwa jamii.
