Na Nishan Khamis
Matemwe Kijini, Wilaya ya Kaskazini ‘A’
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imejipanga kuendelea kuinua vipaji vya vijana kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo katika ngazi za wilaya na mikoa nchini, hatua itakayotoa fursa mbalimbali kwa maendeleo ya sekta ya michezo.
Mhe. Riziki ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakaazi wa Kijiji cha Matemwe Kijini, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha michezo cha wilaya hiyo kinachojengwa katika kijiji hicho.
Amesema ujenzi wa viwanja vya kisasa vya michezo katika ngazi za wilaya na mikoa unaendelea nchi nzima ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Dkt. Mwinyi ya kuimarisha sekta ya michezo, sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2026–2030.
Aidha, ametoa wito kwa wakaazi wa kijiji hicho na wilaya kwa ujumla kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazotekelezwa na serikali, huku akiwahakikishia kuwa changamoto walizowasilisha ikiwemo suala la kiwanja chao cha mazoezi zitafanyiwa kazi, pamoja na fursa za ajira katika ujenzi huo ambapo kipaumbele kitapewa wakaazi wa eneo husika kwa kazi zisizohitaji utaalamu mkubwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Mhe. Badrya Attai Masoud, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, amempongeza Dkt. Mwinyi kwa juhudi kubwa za kimaendeleo katika jimbo hilo. Amesema pamoja na ujenzi wa kiwanja hicho, ujenzi wa barabara ya Matemwe Kijini unaoendelea ni hatua muhimu itakayofungua fursa mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji, wilaya na mkoa kwa ujumla.
Hivyo, amemuomba Waziri wa Habari kuhakikisha kuwa fursa zitokanazo na ujenzi wa kiwanja hicho zinawanufaisha kwa kiasi kikubwa wakaazi wa kijiji hicho, sambamba na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuunga mkono juhudi za maendeleo katika jimbo, wilaya na Zanzibar kwa ujumla.
Nao, wakaazi wa Kijiji cha Matemwe wamesema wamefurahishwa na ujenzi wa kiwanja cha kisasa katika kijiji chao, wakieleza kuwa ni fursa muhimu ya kimaendeleo. Wamehakikishia kuendelea kuunga mkono ujenzi huo, huku wakisisitiza ajira kupewa kipaumbele kwa wakaazi wa eneo hilo pamoja na ujenzi wa kiwanja chao cha mazoezi.
