Popular services

IDDI ALI AME, AMEIPONGEZA CCM JIMBO LA NUNGWI, ATOA ONYO DHIDI YA CHOKOCHOKO JIMBO HILO.

 

Na: Nishan Khamis, Nungwi
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Iddi Ali Ame, ameipongeza CCM Jimbo la Nungwi kwa kuandaa mkutano maalum wa kuwapongeza wajumbe na wanachama wa chama hicho kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana, hali iliyopelekea chama kushinda kwa kishindo jimbo hilo.

Pamoja na pongezi hizo, Mwenyekiti Iddi Ali ameitaka Kamati ya Siasa ya CCM Jimbo la Nungwi kushughulikia kwa haraka chokochoko au viashiria vyovyote vyenye nia mbaya vinavyoweza kuleta mvurugano ndani ya jimbo hilo.

Amesema CCM inaongozwa kwa misingi ya Katiba na Sheria za chama hicho, hivyo amemtaka Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini A kuhakikisha anasimamia ipasavyo na kudhibiti viashiria vyote vinavyoweza kuathiri maendeleo ya jimbo, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.

Aidha, amesema kupitia Ilani ya CCM, mkoa imeelekeza kuimarisha miundombinu bora katika nyanja zote za maendeleo, na kuwataka madiwani, mwakilishi pamoja na mbunge wa Jimbo la Nungwi kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo kwa vitendo zaidi, sambamba na kuimarisha majengo yote ya CCM ya jimbo hilo kwa ushirikiano wa pamoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Nungwi, Ali Mtwana Habibu, amemhakikishia mgeni rasmi kuwa yeye pamoja na Kamati ya Siasa watasimamia ipasavyo na kudhibiti chokochoko au viashiria vyovyote vinavyoweza kutia dosari katika jimbo hilo.

Aidha, ametoa pongezi za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na wanachama wote wa CCM kwa kuhakikisha chama kimeshinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana.

Amesema kama Mwenyekiti wa CCM Jimbo, atasimamia misingi ya Katiba na Sheria za chama, na mtu yeyote atakayebainika kuwa na nia mbaya ya kuruga amani na utulivu wa chama na jimbo hilo kwa ujumla, hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa taratibu.

Ameongeza kuwa mkutano huo ulikuwa maalum kwa ajili ya kuwashukuru wanachama wa Jimbo la Nungwi kwa kazi kubwa waliyoifanya katika uchaguzi uliopita, sambamba na kuadhimisha miaka 49 ya kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi.

Nao madiwani, mwakilishi na mbunge wa Jimbo la Nungwi wametoa pongezi kwa CCM na wananchi kwa ujumla kwa imani kubwa waliyoionesha kwa kuwachagua, huku wakiahidi kutekeleza ahadi walizotoa na kusimamia ipasavyo Ilani ya CCM kwa maendeleo zaidi ya jimbo hilo.

Jumla ya wajumbe 912 kutoka matawi yote ya CCM Jimbo la Nungwi walihudhuria mkutano huo, pamoja na viongozi wa CCM kutoka wilaya na Ofisi Kuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkutano huo ulifanyika katika Uwanja wa Mpira wa Sister Island, Nungwi.