Popular services

 MWANDISHI: Nishan Khamis – Mkwajuni

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ali Amesema, amesema chama hicho kitawasimamia kwa karibu wabunge, wawakilishi na madiwani wa mkoa huo ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa vitendo katika kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030.

Mwenyekiti Iddi Ali Amesema aliyasema hayo jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Jimbo la Mkwajuni, uliolenga kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM kwa kukipa chama ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita. Sambamba na hilo, aliwataka wabunge, wawakilishi na madiwani wa jimbo hilo kueleza kwa vitendo utekelezaji wao katika kipindi cha siku mia moja tangu walipoingia madarakani, hususan miradi na hatua walizochukua kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, kwa kuonesha msisitizo, Mwenyekiti huyo aliwataka viongozi hao kuwasilisha ripoti za utekelezaji kila baada ya miezi mitatu katika majimbo na wadi zao, hatua itakayosaidia chama na wananchi kufuatilia kwa karibu uwajibikaji wa viongozi wao. Vilevile, alitoa pongezi kwa wanachama wa CCM waliojitokeza kwa wingi katika mkutano huo, akisema hali hiyo inaonesha mshikamano na umoja mkubwa ndani ya chama hicho katika jimbo la Mkwajuni.

Hata hivyo, Mwenyekiti Iddi Ali Amesema alikemea vikali vitendo vya kupanga safu za uongozi kuelekea uchaguzi wa mwaka 2030, akiwataka wanachama na viongozi kuacha mara moja tabia hiyo. Alionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo, akisisitiza kuwa chama kinahitaji mshikamano na siyo makundi yanayochochea migawanyiko.

Kwa upande wao, mbunge, mwakilishi na madiwani wa Jimbo la Mkwajuni, wakizungumza katika mkutano huo, wamesema kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazolikabili jimbo hilo ni tatizo la maji. Wamesema tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kuchimba visima katika baadhi ya maeneo, kugawa mipira na matanki ya maji kwa baadhi ya shehia pamoja na kuendelea na taratibu za kukamilisha ujenzi wa kisima kikubwa cha maji kitakachosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.

Viongozi hao wamemuhakikishia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa kwa ushirikiano wao na Serikali Kuu, watahakikisha changamoto zote zilizopo katika jimbo hilo zinasimamiwa ipasavyo na kutatuliwa kwa vitendo kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Nao baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo wametoa pongezi kwa chama kwa kuandaa mkutano huo, wakisema bado kuna changamoto ya maji pamoja na miundombinu ya barabara za ndani. Hivyo wameomba chama, viongozi na serikali kwa ujumla kuharakisha hatua za kuzitatua changamoto hizo ili kuchochea maendeleo endelevu ya wananchi wa jimbo hilo.


Mkutano huo ni mwendelezo wa ziara ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kamati yake ya Mkoa katika majimbo yote ya mkoa huo, kwa lengo la kutoa shukrani kwa wanachama wa chama hicho pamoja na kusikiliza utekelezaji wa viongozi wa CCM katika kipindi cha siku mia moja za uongozi wao. Mkutano wa Mkwajuni umekutanisha matawi yote kumi na manne ya jimbo hilo lililopo Wilaya ya Kaskazini A.