Na Nishan Khamis, Pemba
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Maryam Saidi Khamis, ametekeleza ahadi yake ya kukabidhi msaada wa mifuko 25 ya saruji kwa wanawake wa Madrasa ya Nour Janah iliyopo Kinyasini, Mkoa wa Kusini Pemba, kufuatia ziara yake ya kuwatembelea wanawake hao kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili.Mheshimiwa Maryam alifanya ziara hiyo hivi karibuni ambapo alipata fursa ya kukutana na wanawake wa madrasa hiyo na kusikiliza changamoto zao, hususan changamoto ya miundombinu ya madrasa. Baada ya ziara hiyo, aliahidi kuwasaidia, ahadi ambayo sasa ameitekeleza kwa vitendo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mheshimiwa Maryam Saidi Khamis alisema kuwa dhamira yake ni kuwaunga mkono wanawake katika juhudi zao za kielimu na kijamii, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na jamii katika kuimarisha maendeleo, hasa kwa wanawake na watoto.
Kwa upande wao, wanawake wa Madrasa ya Nour Janah walimpongeza Mheshimiwa Maryam kwa kutimiza ahadi yake kwa vitendo. Kiongozi wa Madrasa hiyo, Bi. Habiba Kassim Mohamed, alimshukuru Mwakilishi huyo wa Viti Maalum kwa msaada huo, akisema mifuko hiyo ya saruji itasaidia kuharakisha ujenzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa madrasa hiyo.

