Popular services

 Na Nishan Khamis, Pemba

MHE. Maryam Said Khamis, Mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Kusini Pemba, amefanikiwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Skuli ya Msingi Buyuni Ndagoni, Mkoa wa Kusini Pemba, hatua iliyopokelewa kwa furaha na pongezi kutoka kwa wananchi, walimu pamoja na wanafunzi wa skuli hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Mhe. Maryam alisema kuwa ni wajibu wa viongozi kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na salama, akisisitiza kuwa maji ni hitaji la msingi katika kulinda afya na kuimarisha maendeleo ya elimu. Alieleza kuwa utekelezaji huo umetokana na ziara yake ya kusikiliza changamoto za wanawake na jamii aliyofanya miezi miwili iliyopita.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Chake Chake, Bi. Halima Juma Khamis, amepongeza juhudi za Mhe. Maryam akisema ni mfano wa uongozi wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa vitendo. Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa katika kuimarisha sekta ya elimu na ustawi wa jamii.

Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Buyuni Ndagoni, Bi. Sada Juma, amesema hapo awali skuli hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa maji, hali iliyokuwa ikiathiri usafi wa mazingira na ratiba ya masomo. Ameeleza kuwa kupatikana kwa maji kutaboresha afya ya wanafunzi na kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.

Katika hatua nyingine, Mhe. Maryam alitoa fedha taslim kwa ajili ya kusaidia mahitaji mbalimbali ya skuli hiyo, jambo lililopokelewa kwa shukrani kubwa na uongozi wa skuli pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Kwa upande wao, wananchi wa Buyuni Ndagoni walitumia fursa hiyo kumuomba Mhe. Maryam kuwasaidia matofali kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya skuli, ombi ambalo Mheshimiwa huyo amelikubali, akiahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa maslahi ya watoto na jamii kwa ujumla.