Popular services

WANANCHI WA JIMBO LA CHAANI WAENDELEE KUNUFAIKA NA NEEMA YA SADAKA YA IFTAR.

 

Na,Nishan khamis, Chaani.
Jumla ya kaya 170  za wananchi wa Jimbo la Chaani zimenufaika na sadaka ya Iftar iliyotolewa kwa makundi maalum ya kijamii wakiwemo watu wenye ulemavu, wazee, mayatima, wajane pamoja na baadhi ya kaya masikini katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Sadaka hiyo imetolewa na taasisi ya huduma kwa jamii, ambapo ilikabidhiwa rasmi na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bwana Arif Surya, akiwa sambamba na Mbunge wa Jimbo la Chaani, Mheshimiwa Ayoub Mohammed Mahmoud ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Kijiji cha Ketwa, Bwana Arif Surya alisema taasisi yake itaendelea kugusa maisha ya wananchi wenye uhitaji, hasa makundi maalum, kwa lengo la kuimarisha ustawi wa jamii na kuendeleza utamaduni wa kusaidiana. Alibainisha kuwa sadaka hiyo ni sehemu ya dhamira ya taasisi katika kurudisha kwa jamii na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Ayoub Mohammed Mahmoud alisisitiza umuhimu wa mshikamano, huruma na ushirikiano kati ya viongozi, taasisi na wananchi ili kuhakikisha makundi yenye uhitaji yanaendelea kupatiwa msaada stahiki.

Aidha, jumla ya shilingi 14,450,000 zimetumika kufanikisha zoezi hilo, likiwa na lengo la kuwapunguzia wananchi wa makundi maalum changamoto za kimaisha na kuwapa faraja katika kipindi hiki cha mfungo. Wananchi waliopokea sadaka hiyo walionesha furaha na shukrani kubwa kwa hatua hiyo, wakiwapongeza viongozi na taasisi kwa kuwakumbuka na kuwasaidia katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.