Popular services

VIONGOZI JIMBO LA CHAANI WATEKELEZA AHADI YA UTOAJI WA RIMU NA WINO KATIKA SKULI ZA MSINGI NA SEKONDARI

 

Na, Nishan Khamis
Viongozi wa Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A, leo wamefanya ziara ya utekelezaji wa ahadi yao ya utoaji wa rimu na wino kwa mashine za fotokopi katika skuli zote za msingi na sekondari za jimbo hilo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Khamis, amesema kuwa kwa ushirikiano na viongozi wengine wa jimbo hilo akiwemo Mbunge wa Jimbo la Chaani, Ayoub Mohammed Mahmoud, Mwakilishi Juma Usonge pamoja na madiwani wote, wameanza kutekeleza ahadi zao walizozitoa kwa wananchi, hususan katika sekta ya elimu.

Amesema lengo la utoaji wa rimu na wino huo ni kuwawezesha wanafunzi kupata mazoezi ya kutosha kupitia mitihani ya majaribio ya mara kwa mara, jambo litakalowasaidia kuwa imara na kujiamini zaidi wanapokabiliwa na mitihani ya kitaifa.

Aidha, ameeleza kuwa huo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa mipango mingine ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa suala la elimu litaendelea kupewa kipaumbele kwa ustawi wa kielimu katika jimbo hilo.

Kwa upande wao, Madiwani wa Viti Maalum wa jimbo hilo wamesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi walizotoa wakati wa kampeni, na wameomba kuendelea kushirikiana na walimu pamoja na jamii kwa ujumla ili kuimarisha maendeleo ya elimu.

Nao walimu, wakipokea vifaa hivyo katika skuli zao, wametoa shukrani za dhati kwa viongozi wa jimbo hilo kwa kutekeleza ahadi zao kwa vitendo. Wamesema vifaa hivyo vilikuwa na uhitaji mkubwa na vitaongeza ufanisi katika utoaji wa mazoezi na mitihani ya majaribio kwa wanafunzi. Pia wameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi katika kutatua changamoto mbalimbali za kielimu.