Popular services

WANAWAKE WAJITOKEZA KWA WINGI KATIKA UCHUKUAJI WA FOMU ZA NAFASI ZA BARAZA LA VIJANA NGAZI YA SHEHIA, WILAYA YA KASKAZINI A

 

Na: Nishan Khamis, Gamba
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Mabaraza ya Vijana ngazi ya shehia Wilaya ya Kaskazini A, Salum Sadoun, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wanawake kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa mabaraza ya vijana shehia wilaya hiyo, ikilinganishwa na miaka iliyopita.


Amesema hapo awali mwitikio ulikuwa mdogo, hususan kwa upande wa wanawake, lakini kwa sasa hali imebadilika na wanawake wengi wamejitokeza kuwania nafasi hizo, jambo linaloonesha kuongezeka kwa uelewa na hamasa ya kushiriki katika uongozi.
Sadoun ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa Kisiwa News Blog katika Ofisi ya Baraza la Vijana Gamba, Wilaya ya Kaskazini A.

Aidha, ametoa wito kwa vijana wote kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za Mwenyekiti, Katibu na wajumbe wa Kamati Tendaji katika ngazi ya shehia, kwa kuzingatia kanuni na taratibu za uchaguzi zilizopo.

Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Vijana Wilaya ya Kaskazini A, Nassor Haji Makame, amesema bado kuna mwitikio mdogo kwa watu wenye ulemavu katika kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo. Hivyo, amewahamasisha kutumia siku chache zilizosalia kujitokeza ili kuhakikisha ushiriki na ushirikishwaji wao katika nafasi za uongozi.

Naye Sanura Nyange Abdalla, mmoja wa wanawake waliojitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana ngazi ya shehia ya Gamba, amesema uamuzi wake umetokana na kuwapo kwa viongozi wanawake nchini wanaoongoza kwa mafanikio, hali iliyompa hamasa ya kuwania nafasi hiyo.

Ametoa wito kwa wanawake wengine kutumia siku zilizobaki kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya vijana, wilaya na mkoa kwa ujumla.

Zoezi la uchaguzi wa Mabaraza ya Vijana kwa shehia zote za Unguja linatarajiwa kufanyika tarehe 21 Februari 2026.