Na: Nishan Khamis, Pwani Mchangani
Mwenyekiti wa Masheha Wilaya ya Kaskazini A, Ussi Haji Baro, amewataka masheha wa wilaya hiyo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo suala la kudumisha usafi katika maeneo yao, ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, za kuimarisha haiba ya usafi Zanzibar.Mwenyekiti Ussi ametoa wito huo leo katika hafla ya usafi iliyofanyika Shehia ya Pwani Mchangani, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kutimiza miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema ni wajibu wa masheha kusimamia harakati zote za kiserikali katika maeneo yao, sambamba na kuwapongeza wananchi pamoja na Baraza la Manispaa kwa ushirikiano wao mzuri katika zoezi hilo la usafi.
Kwa upande wake, Afisa wa Mazingira wa Baraza la Manispaa la Wilaya ya Kaskazini A, Mohammed Hamdu Fadhil, amesema baraza hilo limeweka utaratibu maalum wa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya wilaya, hivyo ni vyema masheha nao wakaandaa na kusimamia ratiba kama hizo ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Amesisitiza kuwa Zanzibar ni kitovu cha utalii, hivyo ushirikiano mkubwa unahitajika katika kutunza na kulinda mazingira.
Naye Sheha wa Pwani Mchangani, Khamis Haji Juma, kwa niaba ya wananchi, ametoa pongezi za dhati kwa masheha hao kwa kujumuika katika zoezi hilo la usafi, na kutoa wito wa kuendelezwa kwa utaratibu huo ili kuweka mazingira safi, hususan ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina shughuli nyingi za kitalii.
