: Nishan Khamis, Gamba
Wadau wa elimu katika Wilaya ya Kaskazini A wametakiwa kushirikiana kwa karibu na wazazi, kamati za skuli pamoja na walimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa wilaya hiyo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Gamba, Mohamed Hassan Hamza, wakati akizungumza katika hafla fupi ya kuwapongeza walimu pamoja na wanafunzi 35 waliofaulu mtihani wa Kidato cha Nne katika Skuli ya Sekondari ya Gamba, iliyopo Wilaya ya Kaskazini A. Hafla hiyo ililenga kutoa hamasa kwa wanafunzi hao kuendelea kufanya vizuri katika hatua zinazofuata za masomo yao.
Amesema wadau wa maendeleo ya elimu wana jukumu kubwa la kuendeleza maendeleo ya vijana katika Wadi ya Gamba, wilaya na mkoa kwa ujumla, iwapo wataendelea kushirikiana katika masuala ya elimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Khamis Makame Khamis, mdau wa maendeleo na Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mkwajuni, amesema Ilani ya CCM inatilia mkazo suala la elimu, hivyo ufaulu wa wanafunzi hao ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa ilani hiyo. Amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya elimu nchini chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Amehakikishia kuendelea kushirikiana na wadau wengine wa elimu ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka zaidi katika skuli hiyo na Wilaya ya Kaskazini A kwa ujumla. Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Gamba, Sabrina Issa Seif, amesema jumla ya wanafunzi 37 walifanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2025, ambapo wanafunzi 35 kati yao wanawake 22 na wanaume 13 walifaulu na kupata sifa ya kuendelea na ngazi mbalimbali za elimu nchini.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uimarishaji wa miundombinu ya elimu, ushirikiano wa wazazi, kamati za skuli, walimu na wadau wa elimu katika wilaya hiyo, pamoja na bidii na nidhamu ya wanafunzi.

