Mwandishi: Nishan Khamis, Kaskazini Unguja
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ (TAMISEMI), Mikidad Mbarouk Mzee, amewataka masheha kusimamia na kushirikiana na jamii katika kuendelea kutunza usafi wa mazingira katika maeneo yao, sambamba na kuimarisha ufahamu wa anuani za makazi katika shehia zao.Amesema hayo leo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo masheha wa mkoa huo kuhusu usimamizi wa masuala ya usafi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuiweka Zanzibar yenye mazingira safi na ya kuvutia.
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya masheha na jamii ni muhimu, hasa kwa kushirikiana na mabaraza ya manispaa na jiji katika harakati za usafi wa mazingira, akibainisha kuwa Mkoa wa Kaskazini Unguja ni wa kitalii, hivyo kuendeleza usafi wa mazingira ni njia bora ya kuendelea kuwavutia watalii na kuongeza pato la taifa.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia masheha kupata uelewa wa kisheria kuhusu majukumu yao, hatua itakayoongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Gallos Nyimbo, amewasihi masheha kuzingatia mafunzo hayo kwa umakini na kuyatumia ipasavyo katika kuimarisha usafi wa mazingira na kuupa mkoa huo haiba nzuri.
Kwa upande wao, masheha wamesema wamefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamewaongezea maarifa mapya katika usimamizi na uwajibikaji wa majukumu yao, na kuahidi kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
