NA NISHAN KHAMIS, MKOKOTONI | TAARIFA: 14 FEBRUARI 2026
Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Dkt. Mahmoud Omar Hamad, amewahimiza wazazi, walimu, wanafunzi pamoja na kamati za skuli kushirikiana ipasavyo katika kuongeza ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi wa jimbo hilo. Pia, amewaomba walimu kuandaa mazingira rafiki mapema ili wanapo fika siku ya kustafu wawe na miradi itakayowawezesha kuendesha maisha yao.Dkt. Mahmoud ameyasema hayo leo katika hafla ya kumuaga Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Mkokotoni Sekondari baada ya muda wake wa kustaafu kufika. Amesema ni wajibu kwa walimu kuandaa mazingira rafiki kabla ya kustaafu, ili wakati wa kustafu utakapofika wawe tayari na wakiwa na njia mbadala ya kuendeleza maendeleo yao katika maisha.
Aidha, amesema ushirikiano baina ya walimu, wazazi, kamati za skuli na wanafunzi ni chachu kubwa ya maendeleo ya elimu katika jimbo hilo. Hivyo, ameomba ushirikiano uendelee ili kuleta ufaulu wenye tija wa daraja la juu, na amewahakikishia walimu na wanafunzi WATAKAOFANYA vizuri katika masomo zawadi maalum kama hamasa ya kuendeleza elimu jimbo la Tumbatu.
Dkt. Mahmoud pia amesema changamoto mbali mbali zilizopo skuli hiyo, ikiwemo maji na masuala ya kambi kwa wanafunzi, amezipokea na kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na viongozi wenzake ili kuimarisha zaidi maendeleo ya kielimu.
Kwa upande wake, Mwalimu mstaafu wa skuli hiyo, Haji Abdalla Seif, ametoa pongezi za dhati kwa mashirikiano makubwa na mafanikio yaliyopatikana katika skuli. Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano kati ya wazazi, walimu, kamati za skuli na wanafunzi, na yanapaswa kuendelezwa ili kuongeza ufaulu zaidi. Pia ametoa shukrani za dhati kwa zawadi ya pikipiki aliyokabidhiwa na walimu wa skuli hiyo.
Walimu, wazazi na wanafunzi pia wametoa pongezi zao kwa mwalimu mstaafu na kumuomba kuendelea kushirikiana nao katika harakati za kuendeleza elimu jimbo hilo. Vilevile, wamemuomba Mwakilishi na viongozi wengine wa jimbo hilo kuendelea kushirikiana ipasavyo ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa kuandaa mazingira bora ya kufikia ndoto zao za maisha.

