Popular services

 Na Nishan Khamis, Chaani

Taasisi ya Sister Island imetoa sadaka ya vyakula na mavazi kwa Jumuiya ya Watu Wasioona Wilaya ya Kaskazini A, hafla iliyofanyika leo katika ofisi za jumuiya hiyo zilizopo Chaani, Lungalunga.

Sadaka hiyo imetolewa ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wanajumuiya hao katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan sambamba na kuwasaidia kupata mavazi kwa ajili ya Sikukuu ya Eid.

Akizungumza wakati wa kukabidhi sadaka hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sister Island, Francesca Michael, amesema kuwa yeye ni sehemu ya jamii na anatambua changamoto mbalimbali za kijamii zinazowakabili wananchi, huku akieleza kuwa utoaji wa sadaka hiyo ni sehemu ya muendelezo wa taasisi hiyo katika kusaidia jamii katika harakati mbalimbali za maendeleo nchini.

Kwa upande wake, Mhasibu wa taasisi hiyo, Haji Moh’d Ali, amesema jumla ya kilo 300 za mchele, kilo 100 za njugu pamoja na mavazi ya watoto na watu wazima vimetolewa kwa jumuiya hiyo. Aidha, ameupongeza uongozi wa jumuiya kwa ushirikiano mzuri na kuwaomba kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali kwa lengo la kuunga mkono juhudi za maendeleo ya wananchi.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Watu Wasioona Wilaya ya Kaskazini A, Fatma Mngwali Khamis, ameishukuru Taasisi ya Sister Island kwa sadaka hiyo akisema itawasaidia kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan, huku akiomba kuendelea kusaidiwa katika changamoto nyingine kwa ajili ya kuimarisha jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Khamis, amewashukuru wahisani hao kwa sadaka waliyoitoa na kuwahakikishia kuwa viongozi wa jimbo hilo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na Serikali, wanaendelea kushirikiana kwa karibu katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.