Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Kusini Pemba, Zuwena Abdalla Haji, amewataka wanawake wa jumuiya hiyo katika Wilaya ya Mkoani kushikamana, kudumisha upendo na kutunza rasilimali za jumuiya ili kuendeleza maendeleo ya UWT na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ujumla.
Akizungumza katika ofisi za CCM Wilaya ya Mkoani wakati wa hafla ya kukabidhiwa mashine ya fotokopi, Mwenyekiti Zuwena alisema mashine hiyo imekabidhiwa na Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mheshimiwa Maryam Said Khamis, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi.
Alisema ushirikiano na mshikamano ni nguzo muhimu ya maendeleo ya UWT na chama kwa ujumla, huku akiwataka wanachama kuitunza mashine hiyo yenye thamani kubwa ili iwe chachu ya maendeleo zaidi. Aidha, alimpongeza Mheshimiwa Maryam kwa jitihada zake za utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo, akisema ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine katika kuwaletea wanachama maendeleo.
Kwa upande wake, akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Maryam Said Khamis alisema mashine ya fotokopi aliyokabidhi ina thamani ya shilingi milioni saba, na imepatikana kutokana na ushirikiano wa Kamati Tendaji ya UWT baada ya kukaa pamoja na kutafakari namna bora ya kusherehekea miaka 49 ya CCM kwa vitendo.
Aliongeza kuwa ataendelea kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, sambamba na kuwaomba wanachama wa UWT na CCM kwa ujumla kuwaendeleza dua Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, pamoja na kuwaunga mkono ili waendelee kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Kwa upande wao, wajumbe wa UWT Wilaya ya Mkoani walitoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Maryam Said Khamis kwa kuipatia jumuiya hiyo mashine ya fotokopi, wakisema itarahisisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi kutokana na uwepo wa kifaa hicho cha kisasa. Aidha, walimhakikishia kuwa wataitunza na kuithamini mashine hiyo kwa maendeleo endelevu ya jumuiya na chama kwa ujumla.

