Popular services

 Na,Nishan khamis, Gamba.

Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Zainab Khamis Shomar, amewataka Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Kaskazini Unguja kuhakikisha wanatekeleza ahadi ya kujenga majengo ya umoja huo kwa ajili ya maendeleo ya jumuiya na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti ameyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika nyumba ya mtumishi wa UWT Wilaya ya Kaskazini A, iliyopo Gamba, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977.

Aidha, amewahimiza vijana kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi, akisisitiza kuwa ni chama pekee kinachopeleka mbele maendeleo ya nchi kwa kudumisha amani na utulivu, misingi mikuu ya maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.

Halikadhalika, ametoa pongezi za dhati kwa ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa na jumuiya pamoja na viongozi mbalimbali waliochangia kwa hali na mali katika ujenzi huo, huku yeye mwenyewe akichangia shilingi milioni mbili kama ishara ya kuunga mkono juhudi za kukamilisha ujenzi huo.

Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa nyumba hiyo, Katibu wa UWT Wilaya ya Kaskazini A, Mtenge Makame Faki, amesema ujenzi huo ulianza tarehe 10 Juni, 2010 kwa wazo la wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT wilaya hiyo. Ameeleza kuwa gharama za ujenzi hadi kukamilika zinakadiriwa kufikia shilingi milioni themanini laki tatu elfu nne mia tano na sitini (80,304,560), ambapo hadi sasa zimetumika shilingi milioni hamsini laki moja elfu tatu na thelathini na tano (50,103,035).

Aidha, ametoa pongezi kwa viongozi wa CCM pamoja na viongozi wa Serikali wa mkoa na wilaya, wabunge, wawakilishi na madiwani kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa katika kufanikisha ujenzi huo.

Akitoa neno la shukrani katika hafla hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UWT Wilaya ya Kaskazini A, Rahma Abdalla Maisara, amempongeza mgeni rasmi kwa kushiriki hafla hiyo na amemhakikishia kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa maslahi ya jumuiya na chama kwa ujumla.