Na Nishan Khamis, Chaani
Mwakilishi wa Jimbo la Chaani, Mhe. Juma Hamad Usonge, amewataka wazazi wa jimbo hilo kuyapokea mabadiliko ya mitaala ya elimu nchini kwa lengo la kuleta maendeleo mapana katika sekta ya elimu na kuwawezesha wanafunzi kupata elimu yenye tija itakayowaandaa vyema kwa soko la ajira au kujiajiri.
Mhe. Usonge ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika kikao cha wazazi, walimu na wanafunzi kilichofanyika katika Skuli ya Sekondari Kinyasini, Wilaya ya Kaskazini A. Kikao hicho kililenga kujadili masuala ya elimu na kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa skuli hiyo.
Katika maelezo yake, aliwatoa hofu wazazi, walimu na wanafunzi kuhusu mabadiliko ya mitaala, akieleza kuwa serikali ina dhamira njema ya kuboresha elimu ili kumjenga mwanafunzi kitaaluma na kimaarifa zaidi, sambamba na mahitaji ya soko la ajira la sasa.
Aidha, amewahakikishia kuwa viongozi wa jimbo hilo wataendelea kushirikiana kuhakikisha elimu inaimarika zaidi. Amesema tayari wiki iliyopita waligawa rim za karatasi na wino wa mashine za fotokopi kwa skuli zote tisa za msingi na sekondari katika jimbo hilo ili kusaidia maandalizi ya wanafunzi.
Ameongeza kuwa baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Ramadhani, wataanza kutoa chakula kwa wanafunzi wa kambi bila ya mzazi kuchangia gharama yoyote, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yao ya kampeni yenye lengo la kukuza elimu bora kwa vijana wa jimbo hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Chaani, Khamis Haji Khamis, amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imejipanga kuweka mazingira bora ya kielimu nchini. Ameeleza kuwa ni vyema jamii ikaunga mkono juhudi hizo ili kufikia maendeleo ya kielimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika skuli za jimbo hilo.
Nao wazazi na walimu waliohudhuria kikao hicho wametoa pongezi kwa ushirikiano wa viongozi wa jimbo hilo na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya ufaulu katika skuli hiyo. Hata hivyo, wameomba kutatuliwa changamoto ya ukosefu wa mwalimu wa masomo ya Uhasibu na Biashara.
