Uwandani, Pemba —
Mwakilishi wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Maryam Said Khamis, ametekeleza ahadi yake kwa kuwanunulia mipira ya maji wanawake wakulima wa mboga mboga wa Uwandani, hatua inayolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuboresha uzalishaji wa kilimo.Utekelezaji wa ahadi hiyo umefanyika baada ya Mhe. Maryam kufanya ziara za kusikiliza changamoto za wanawake katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kusini Pemba, ambapo wanawake wakulima wa Uwandani waliwasilisha changamoto ya uhaba wa maji kwa shughuli za umwagiliaji, hali iliyokuwa ikiathiri uzalishaji na kipato chao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mipira hiyo, Mhe. Maryam alisema kuwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii, akisisitiza kuwa changamoto zinazowasilishwa na wananchi zinapaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo.
“Wanawake ndio uti wa mgongo wa familia na jamii. Niliposikiliza changamoto zao, suala la maji lilijitokeza kuwa kikwazo kikubwa katika kilimo cha mboga mboga. Hivyo nimeamua kutekeleza ahadi niliyotoa ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao,” alisema Mhe. Maryam.
Wanawake wakulima wa Uwandani waliupokea msaada huo kwa furaha, wakimshukuru Mwakilishi huyo kwa kutimiza ahadi kwa vitendo, na kueleza kuwa mipira ya maji itarahisisha umwagiliaji wa mashamba yao, kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato cha familia zao.
Kwa upande wao, viongozi wa eneo hilo walisema hatua hiyo ni chachu ya kuimarisha kilimo cha mboga mboga na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii, huku wakitoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanawake.
Mhe. Maryam Said Khamis ameahidi kuendelea kuwa karibu na wanawake na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba kwa lengo la kusikiliza na kushughulikia changamoto zao, hususan katika sekta za kilimo, maji na ustawi wa jamii, ili kufikia maendeleo endelevu.
